WIZARA ya Nishati na Madini imeshauriwa kuifutia leseni Kampuni
ya uchimbaji wa madini ya SHANTA GOLD MINES CO LTD inayofanya shughuli zake
katika kata ya Mang’onyi, wilayani Ikungi,Mkoani Singida kutokana na kushindwa
kuanza uchimbaji huo na badala yake leseni hiyo itolewe kwa wawekezaji wengine
ili kuepuka malumbano yasiyokuwa na msingi na Kampuni hiyo.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa wilaya ya Ikungi,BWANA MIRAJI
MTATURU katika Kijiji cha Murumbi,Kata ya Mang’onyi,wilayani humo wakati wa
ziara ya kutembelea na kukagua shughuli za uchimbaji wa madini ya aina mbali
mbali unaoendelea katika wilaya hiyo.
Aidha BWANA MTATURU amesisitiza kwamba serikali wilayani Ikungi
haina sababu ya kuendelea na malumbano ya miaka mingi ambayo hayana sababu na
endapo inaonekana Kampuni hiyo imeshindwa kufanya kazi hiyo ni vyema wakafutiwa
leseni na kupewa wawekezaji wengine ambao wapo tayari kufanya kazi hiyo.
Hata hivyo BWANA MTATURU ametumia fursa hiyo kuwaalika
wawekezaji wengine ambao wanaweza kwenda kuwekeza kwani wilaya hiyo ina dhahabu
yenye asilimia 91 hadi 96,ni dhahabu yenye kiwango cha juu kuliko dhahabu
yeyote nchini.
BWANA MTATURU ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na
usalama wa wilaya hiyo hata hivyo ametumua ziara hiyo kukemea siasa zinazorudisha
nyuma maendeleo ya wilaya hiyo na kwamba hazitavumiliwa na kwa yeyote yule
atakayebainika kutumia majukwa ya kisiasa atachukuliwa hatua za kisheria.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa wachimbaji madini Mkoa wa Singida
(SIREMA)BWANA ROBERT MARANDO amesema mgodi wake una mashimo 47 lakini
mashimo yanayozalisha ni matatu na ameajiri wafanyakazi 130 wenye mikataba na
kwamba baadhi yao ni wanakijiji wasiopenda kufanyakazi ngumu.
0 Comments