Wabunge wote wa vyama vya upinzani waliokuwa bungeni katika
kikao kinachoendelea jioni hii wametoka nje ya Bunge, wakipinga wenzao
kufukuzwa bungeni pamoja na kitendo cha Mbunge Tundu Lissu kukamatwa.
Wabunge waliokuwa wameamuliwa kutoka nje ya ukumbi wa Bunge na
Naibu Spika Dkt Tulia Ackson ni pamoja na mbunge wa Kawe Halima Mdee, Mbunge wa
Bunda Mjini Ester Bulaya na Mbunge wa Serengeti Marwa Ryoba.
Wabunge hao watatu wamedaiwa kupinga uamuzi wa Naibu Spika
kuhusu muongozo ulioombwa na mbunge wa Kigoma Mjini Zitto Kabwe, kuhusu
utaratibu uliotumika kumkamata mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.
Mara baada ya Naibu Spika kutoa maamuzi ya kuwaondoa wabunge hao
watatu bungeni, ndipo wabunge wengine wa upinzani pia wakaamua kutoka kama
ishara ya kupinga maamuzi hayo, pia ikiwa ni ishara ya kupinga utaratibu wa
kukamatwa kwa mbunge Tundu Lissu.
Nje ya ukumbi wa Bunge, Mbunge wa Kigoma Mjini Zitto Kabwe ,
amesema wamefikia hatua hiyo kuonesha kuwa uataratibu unaotumiwa kukamata
wabunge wakiwa bungeni siyo sahihi, na kwamba kesho wataendelea na vikao vya
bunge lakini mapambano yataendelea.
"Kesho tunarudi bungeni, lakini mapambano yataendelea,
tunataka kuonesha kuwa utaratibu huu wa kuvizia wabunge kwenye milango ya bunge
bila taarifa rasmi ya Spika na bila kuwaeleza wabunge sababu za kukamatwa kwao
siyo sawa. Tukilifumbia macho litakuja kumtokea mbunge yoyote hata wa CCM"
Amesema Zitto.
0 Comments