MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Thomas Emmanuel Ulimwengu
anaondoka nchini leo kwenda kukamilisha usajili wake klabu ya AFC Eskilstuna ya
Ligi Kuu ya Sweden.
Ulimwengu amesema kwamba baada ya mazungumzo ya awali na klabu hiyo
anakwenda kusaini mkataba wa miaka miwili na klabu hiyo, ambayo awali ilikuwa
inajulikana kama FC Cafe Opera na Vasby United.
“Napenda kutoa shukrani
zangu za dhati kwa watu wangu wote wa karibu kama Jamal Kisongo ambao wamekuwa
karibu na mimi kwa kipindi chote hiki na kunipa ushauri hadi kufikia maamuzi
haya ya kujiunga na timu hii. Tumekataa ofa nyingi sana na kuikubali hii kwa
sababu za msingi sana,”alisema.
Ulimwengu alisema kwamba anashukuru Mungu ndoto zake za kucheza Ligi Kuu
Ulaya zinatimia na ataitumia AFC Eskilstuna kama daraja la kupandia timu kubwa
barani humo.
“Kila kitu ni malengo tu, inategemea na mtu unataka kitu gani katika
wakati gani, nakwenda AFC Eskilstuna kucheza mpira kama nilivyocheza TP Mazembe
ili nionekane nisogee mbele zaidi,”alisema.
Ulimwengu aliyezaliwa Juni 14, mwaka 1993 aliibukia katika taasisi ya
soka Tanzania (TSA) mwaka 2008, kabla ya mwaka 2009 kwenda kuanza kukomazwa
Ligi Kuu katika klabu ya Moro United alikokuwa akicheza kwa mkopo hadi mwaka
2010 alipokwenda akademi ya Athletic FC ya Sweden, alikocheza hadi 2011 TP
Mazembe alipochukuliwa na timu ya vijana ya Mazembe.
Alicheza U-20 ya Mazembe kwa msimu moja kabla ya kupandishwa rasmi timu
ya wakubwa mwaka 2012 na moja kwa moja kuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza hadi
anamaliza Mkataba wake Oktoba mwaka jana.
Ulimwengu anajivunia kushinda mataji makubwa akiwa na Mazembe kama
Ligi ya Mabingwa Afrika, Super Cup ya Afrika na pamoja na kucheza Klabu Bingwa
ya Dunia.
0 Comments