ENDESHI FC MABINGWA PUNDA CUP 202O

 

Na Cales Katemana

Singida.

Vijana wamelipongeza Shirika la Inades formation kwa kuibua vipaji kwa Vijana katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida kupitia Mradi wao wa kuihimiza jamii kumthamini Mnyama kazi Punda kama wanyama wengine.

Akizungumza mara baada ya kumalizika mchezo wa mpira wa miguu 'Punda Cup' wa fainali ulioshirikisha timu za Mumbii,Mwachambia,Ghata na Endesh nahodha wa timu ya Endesh Fc ambayo imeibuka kidedea Paul Elias alilipongeza shirika hilo kwa kuanzisha mashindano hayo.

"Kwakweli mashindano haya ni mazuri licha ya kulenga kufikisha ujumbe kwa jamii kumthamini punda pia yanaibua vipaji vya vijana ingizingatiwa sisi huku tuko vijijini sio rahisi sana vipaji vyetu kuonekana lakini kupitia haya mashindano vipaji vinaenda kuonekana." alisema Nahodha huyo na kuongeza.

"Ni kweli Punda anatusidia sana kwahiyo kutokana na elimu hii tuliyoipata naomba tumtunze ili atutuze,tuache kuwauza wataisha na tutabakia kuwaona kwenye picha tu." 

Katika mashindano hayo mshindi wa kwanza alipewa mipira miwili na jezi na wapili alipata mipira miwili huku mshindi wa tatu akipata mpira mmoja, mchezo uliopigwa katika viwanja vya CCM kata ya Msange wilayani Singida Dc.

Afisa mifugo na uvuvi Wilaya hiyo ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mashindano hayo Theophil Ishengoma aliwapongeza vijana hao na kuwaomba kutojiingiza kwenye makundi mabaya badala yake wajiingize kwenye fursa mbalimbali kama hizi za kucheza mpira wa miguu.

Alisema lengo kubwa la mashindano hayo yanalenga kuielimisha jamii kumthamini punda hivyo akawataka vijana hao na jamii kwa ujumla kuufanyia kazi ujumbe huo.

"Michezo ni ajira, Vijana jihusisheni na michezo hii,nawaomba pia vilabu mbalimbali nchini kutafuta vipaji huku vijijini wapo Vijana wazuri huku." alisema Ishengoma.

Kwa upande wake Fadhil Geofrey aliyemwakilisha Mkurugenzi wa Shirika hilo alisema waliamua kutumia michezo hususani mchezo wa mpira wa miguu katika kufikisha ujumbe kwa jamii juu ya umuhimu wa mnyama punda kwa jamii.

"Vijana mlioshiriki mashindano haya nawaomba mkaendelee kuifikisha elimu hii huko mnakokaa na tutaandaa mashindano mengine mda sio mrefu hivyo mjipange ili muinue vipaji vyenu." alisema.

 

 

Tuandikie Maoni Yako Hapa

Post a Comment

0 Comments