JANVIER Bokungu ameingia rasmi kwenye
orodha ya mashujaa wa timu ya Simba baada ya kuisaidia kutinga fainali ya kombe
la Mapinduzi kwa kuwafunga watani wao wajadi Yanga kwa mikwaju ya penalti 4-2
kutokana na sare ya bila kufungana katika muda wa kawaida kwenye mchezo wa nusu
fainali ya pili iliyopigwa uwanja wa Amani.
Licha ya kufunga penati ya ushindi,
beki huyo mtulivu aliokoa mipira miwili iliyokuwa ikielekea nyavuni huku pia
akizuia krosi kadhaa ambazo zingeweza kuwa na madhara langoni mwao.
Mlinda mlango Daniel Agyei aliokoa
penati mbili zilizopigwa na Deogratius Munishi na Mwinyi Haji huku mwenyewe
akifunga mkwaju wa pili. Beki Method Mwanjale alikosa mkwaju wake kwa upande wa
Simba.
Nahodha Jonas Mkude na Mzamiru Yassin
wao walifunga penati zao huku Simon Msuva na Thabani Kamusoko wakifunga kwa
upande wa Yanga.
Kwa maana hiyo Simba ambayo ni
mabingwa mara tatu wa michuano hiyo itacheza fainali na Azam FC siku ya Ijumaa
huku wenyewe wakitinga fainali baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya
Taifa Jang'ombe kwenye mchezo wa nusu fainali ya kwanza iliyopigwa jioni.
Mchezo huo ulianza kwa kasi kiasi
ambapo timu zote zilishambuliana kwa zamu huku zikicheza kwa tahadhari kubwa
kuhakikisha nyavu zao hazitikiswi na mpira ukichezwa zaidi eneo la katikati ya
uwanja.
Kiungo Mohammed Ibrahim wa Simba
alipata nafasi ya kufunga dakika ya 43 na shuti lake la mguu wa kushoto
likagonga mwamba huku Juma Liuzio akishindwa kumalizia baada ya mpira kumfuata
mguuni.
Kocha wa Simba Joseph Omog ambaye muda
mwingi wa mchezo alikuwa amesimama kutoa maelekezo kwa wachezaji wake aliwatoa
Shiza Kichuya,Liuzio na Ibrahim nafasi zao zikachuliwa na Jamal Mnyate, Pastory
Athanas pamoja Laudit Mavugo huku Yanga ikimuingiza Emmanuel Martin kuchukua
nafasi ya Deus Kaseke.
Huu unakuwa mchezo wa tano baina ya
timu hizo kukutana kwenye uwanja huo ambapo Simba wameshinda mechi nne na Yanga
wakiibuka na ushindi mara moja.
0 Comments