Rais wa Uganda Yoweri Museveni
amemteua mwanawe Meja Jenerali Muhoozi Kainerugaba, kuwa mshauri mkuu wa rais
kuhusu operesheni maalum.
Mke wa Museveni, Bi Janet Kataaha Museveni ni Waziri wa Elimu na
Michezo, wadhifa ambao alikabidhiwa Juni mwaka jana.
Jenerali Kainerugaba amekuwa kamanda wa kikosi maalum cha
wanajeshi (SFC) chenye jukumu la kutekeleza operesheni maalum za kijeshi.
Kikosi hicho husimamia ulinzi wa rais na kulinda maeneo muhimu
kwa serikali Uganda.
Luteni kanali Don Nabaasa amepandishwa cheo na kuwa kanali na
akateuliwa kaimu kamanda wa SFC.
Rais Museveni pia amemteua mkuu mpya wa
majeshi, Meja Jenerali David Muhoozi ambaye amepandishwa cheo na kuwa jenerali.
Mkuu wa majeshi wa awali, Jenerali Edward Katumba Wamala
amehamishwa na kuteuliwa waziri wa ujenzi.
Kwenye mabadiliko hayo yaliyotangazwa na msemaji wa Majeshi ya
Ulinzi ya Uganda (UPDF) Luteni Kanali,
Rais Museveni amempandisha afisa mkuu wa majeshi aliyeongoza operesheni
ya kushambulia ikulu ya mfalme wa Rwenzururu, magharibi mwa nchi hiyo.
Watu 100 walifariki wakati wa operesheni hiyo.
Mfalme wa Rwenzururu Charles Wesley Mumbere alikamatwa na bado anazuiliwa.
Brigidia Peter Elwelu, aliyekuwa mkuu wa
kikosi cha wanajeshi hao wenye kambi yao kuu Mbarara, amepandishwa cheo na kuwa
meja jenerali na akateuliwa kamanda wa majeshi ya nchi kavu.
0 Comments