Serikali ya Tanzania imesema mzozo
kuhusu mpaka wake na Malawi katika Ziwa Malawi kwa sasa unashughulikiwa na jopo
la maais wastaafu, na kwamba uhusiano kati ya nchi hizo mbili umeimarika.
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
kupitia taarifa, imesema kwamba licha ya kuwepo kwa mgogoro wa mpaka wa
Tanzania na Malawi katika Ziwa Nyasa, uhusiano wa nchi hizo mbili ni mzuri.
"Ukweli ni kuwa, mgogoro wa mpaka kati ya Tanzania na
Malawi kwa sasa upo chini ya Jopo la Viongozi Wastaafu wa Afrika wanaotokea
kwenye nchi za Ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC),"
taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imesema.
"Jopo hilo linaongozwa na Joachim Chissano, Rais Mstaafu wa
Msumbiji akisaidiwa na Festus Mogae, Rais Mstaafu wa Botswana na Thabo Mbeki,
Rais Mstaafu wa Afrika Kusini."
Taarifa hiyo ya serikali imetolewa baada ya wasiwasi kutanda
kuhusu uwezekano wa kuzuka tena kwa mzozo kati ya nchi hizo kutokana na ramani
iliyodaiwa kutolewa na Tanzania ikionyesha kuwa inaamiliki nusu ya Ziwa Malawi
au Nyasa.
Ramani hiyo ya Tanzania ilionyesha kuwa eneo la Kaskazini
Mashariki mwa ziwa hilo ni sehemu ya himaya yake, lakini Malawi nayo inadai
kuwa eneo hilo lote ni lake.
0 Comments