Dr Rehema Nchimbi mkuu wa mkoa mpya wa Singida (picha kutoka maktaba) |
MKUU mpya wa mkoa wa
Singida,Dk.Rehema Nchimbi,amemwagiza mkuu wa wilaya ya
Manyoni na OCD wake, ndani ya mwezi moja wawe wamefanya uchuguzi wa
kina kujua chanzo cha moto ulioteketeza bweni la wasichana shule
sekondari Mwanzi mjini hapa.
Amesema chanzo cha moto
huo ni lazima kijulikane mapema,ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kukomesha
vitendo vya uchomaji moto mabweni.
Mkuu huyo wa mkoa,ametoa
agizo hilo juzi muda mfupi baada ya kukagua ujenzi unaoendelea wa bweni la
wasichana wa kidato cha tano na sita sekondari ya Mwanzi.
Alisema ni jambo la
kushangaza na kusikitisha jeshi la polisi kuchukua muda mrefu (miezi
mitatu) bila kubaini chanzo cha moto ambao pamoja na kuteketeza jengo la
mbweni,umeteketeza pia mali zote,madaftari na vifaa vyote vya kujifunzia vya
wanafunzi.
“Jeshi la polisi
ninalolifahamu mimi hufanya mambo makubwa na mazuri kwa kipindi kifupi.Sasa
hili jambo ambalo sio kubwa la kuchunguza chanzo cha moto uliounguza bweni
hili,kwa nini umechukua mrefu kiasi hiki”,alihoji Dk.Nchimbi na kuagiza
uchunguzi huo ukamilike ndani ya mwezi moja.
Katika hatua
nyingine,mkuu huyo wa mkoa,ametumia fursa hiyo kulishukru shirika la
nyumba taifa (NHC) kwa msaada wake wa mifuko ya saruji 10,kofia za
bati 20,mabati 90 geji 28 vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya shilingi 2.6
milioni.Msaada huo ni kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa bweni la sekondari
Mwanzi.
Aidha,Dk.Nchimbi ametoa
wito kwa mashirika,watu binafsi na taasisi zikiwemo mabenki,kuiga mfano mzuri
wa NHC kusaidia serikali katika kuboresha sekta mbalimbali ikiwemo ya elimu.
“Mimi nitumie nafasi hii
kuwaita au kuwaalika mabenki na taasisi zingine kuja mkoani Singida kutuunga
mkono katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ya wananchi, pamoja na
uboreshaji wa miundo mbinu ya shule za msingi na sekondari”,alisema.
Alisema benki ,shirika
au watu binafsi watakaojitokeza kuunga mkono kuuendeleza mkoa wa Singida kwa
kujenga jengo lo lote pamoja na majengo ya shule,huduma za afya na
mengine yanayolenga kuwanufaisha wananchi,wataruhusiwa kupaka rangi zao na
kuweka nembo zao.
“Kwa upande wa wadau
binafsi,na wao wataruhusiwa kuweka picha za familia zao kwenye majengo au
miradi husika.Kama ni mfugaji na ameuza sehemu ya mifugo yake kugharamia miradi
wa umma,ataruhusiwa kuweka picha ya familia na ng’ombe zao”,alisema Dk.Nchimbi.
Alisema kwa njia
hiyo,benki,taasisi au watu binafsi watakuwa wamejitangaza na tangazo hilo
litadumu kwa muda mrefu ikilinganishwa na matangazo mengi.
Kwa upande wake mkuu wa
wilaya ya Manyoni Geofrey Mwambe,alisema wakati wanaendelea na ujenzi wa
bweni,wamejipanga pia kujenga uzio katika shule hiyo ya sekondari ya
Mwanzi.
“Mheshimiwa mkuu wa
mkoa,shule hii kutokuwa na uzio,kumesababisha madhara mengi ikiwemo wanafunzi
sita wa kike kubebeshwa mimba. Kati yao watano,wamebebeshwa mimba na madereva
WA boda boda.Tunatarajia ujenzi wa uzio uanze mapema iwezekanavyo”,alisema
Mwambe.
Wakati huo huo, meneja
wa NHC mkoa wa Singida,Ladislaus Bamanyisa,amesema wataendelea kuiunga mkono
serikali katika kuboresha sekta mbalmbali elimu ikiwemo.
taarifa na Gersper Endru
0 Comments