Gazeti la Tanzania Daima limeripoti kuwa Serikali imeanza
uhakiki wa vyeti vya ndoa kwa watumishi wa umma. Hatua hiyo ambayo imewashtua
watumishi wengi wa umma, imeelezwa kuwa ni mwendelezo wa harakati za Serikali
ya Rais John Magufuli kuhakiki watumishi wa umma ili kuondokana na watumishi
hewa.
Wakati Serikali ikianza na uhakiki wa vyeti vya ndoa, kazi ya
uhakiki wa watumishi hewa na vyeti vyao vya elimu inaendelea sehemu mbalimbali
nchini.
Kwa muhibu wa Gazeti hilo, habari ambazo limezipata zinasema
kuwa serikali imeanzisha uhakiki huo nchi nzima kwa madai kuwa baadhi ya
watumishi wa umma wamekuwa wakitoa taarifa za uongo kwamba wana ndoa ili kupata
nauli na stahiki zingine za likizo wakati hawana ndoa.
Habari zaidi zinasema kuwa walimu wakuu wa shule zote za Wilaya
ya Ilala wamepewa siku mbili kutekeleza agizo hilo kwa walimu wao.
Mmoja wa walimu hao ambaye ameomba jina lake lihifadhiwe,
alilithibitishia Tanzania daima kuwa ametoa siku mbili kwa walimu wa
shule yake wenye vyeti vya ndoa waviwasilishe kwake.
"Kweli tumepewa agizo hilo leo manispaa ya Ilala na
tumetakiwa kuwasilisha vyeti hivyo kesho na tayari baadhi ya walimu wangu
wamefanya hivyo leo na kesho zoezi hilo linakamilika"
Alipoulizwa sababu ya kuwepo kwa zoezi hilo, mwalimu huyo
alisema hajui lakini anahisi lina lengo la kudhibiti taarifa za uongo za
watumishi wakati wa kuomba likizo.
Wakati walimu wa shule za Ilala wakitakiwa kuwasilisha vyeti
vyao vya ndoa, wilaya nyingine za Temeke, Kinondoni, Ubungo na Kigamboni hawana
taarifa hizo.
Mmoja wa walimu kutoka Manispaa ya Ilala alisema kuwa uhakiki
huo una lengo la kutaka kuchelewesha zaidi malipo na stahiki za walimu za
likizo ambazo hazijalipwa kwa miaka mingi.
0 Comments