SERIKALI imeombwa
kuwaondoa baadhi ya watu wasiokuwa na sifa za kupewa ruzuku kupitia Mpango wa
kunusuru kaya maskini (TASAF) ili watu wanaostahili kunufaika na mpango huo
waweze kupokea fedha zinazotolewa na mpango huo.
Ombi hilo limetolewa na
baadhi ya wajumbe wa Baraza la Mamlaka ya Mji mdogo wa Igunga,Mkoani Tabora
kwenye kikao cha baraza hilo kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri hiyo.
Wakichangia kwa nyakati
tofauti,wakati wa kikao hicho cha baraza,mmoja wa wajumbe hao,Bwana Kulwa
Fideli na Bwana Abeli Mpinga wamebainisha kwamba kuna baadhi ya watu wana
maduka,lakini jambo la kushangaza na kusikitisha ni kuwa wananufaika wa mpango
huo.
Wameweka wazi mbele ya
kikao hicho wajumbe hao kuwa kuendelea kunufaika na mpango huo kwa watu hao
wenye uwezo kifedha,kunawanyima baadhi ya walengwa wasiokuwa na uwezo.
Kwa upande wa Bwana
Kulwa amesema ni vema serikali ikaangalia uwezekano wa kuwaondoa watu wa aina
hiyo ili nafasi za misaada hiyo iweze kutumika kwa walengwa walioachwa katika
orodha ya watu wanaotakiwa kunufaika.
Naye Bwana Abeli Mpinga
ametanabaisha pia kuwa wao kama wenyeviti wa serikali za Mitaa wameshawahi
kutoa elimu kwa wananchi kwa kushirikiana na viongozi wa TASAF,lakini cha ajabu
ni kuwa wananchi ndiyo wamekuwa wakiwaingiza baadhi ya watu wenye uwezo.
Akijibu hoja za
malalamiko hayo kwenye baraza hilo,Mratibu wa Mpango wa kunusuru kaya masikini
(TASAF ) wilaya ya Igunga,Bi Dina Madeje amekiri kuwepo kwa baadhi ya watu
wasio na sifa za kuwepo katika mpango huo.
Hata hivyo Mratibu huyo
amesisitiza pia kwamba jumla ya watu 92 tayari wameshaondolewa katika mpango
huo,na kwamba kati ya idadi ya watu hao,41 wamebainika kuwa hawana sifa
wakiwemo watu 36 waliohama na watu wengine 15 waliofariki na kuongeza kuwa
zoezi la kuwabaini wasio na sifa ni endelevu.
0 Comments