Mch Getrude Rwakatare |
Mchungaji
Kiongozi wa Kanisa la Assemblies of God (Mlima wa Moto), Getrude Rwakatare
amesema ataendelea na mpango wake wa kuwanusuru wafungwa wanaotumikia adhabu
magerezani kwa kuwalipia faini ili warejee uraiani.
Akizungumza na
waandishi wa habari jana Dar es Salaam, alisema katika awamu ya pili ameamua
kuwalipia wafungwa 43 waliopo katika magereza ya Mkoa wa Dodoma.
“Kampeni hii ya kuwalipia faini kati ya Sh 50,000 hadi 200,000 wafungwa
waliopo magerezani imetupa moyo na Watanzania wengi wameguswa na hata
kutupongeza. Kutokana na hali hii kanisa letu sasa limefanya hivyo tena na
safari hii tunaelekea mkoani Dodoma,” alisema.
Mchungaji Rwakatare
alisema kesho watawatoa wafungwa hao mkoani Dodoma ambapo vigezo walivyoangalia
ni wanawake wanaonyonyesha, wagonjwa na wazee.
“Nasi tunatimiza maandiko ya Mungu katika kufanya hivi na kuunga mkono
juhudi za Mwenyekiti wa Parole, Augustino Mrema,” alisema Mchungaji Rwakatare.
Alisema kutokana na
makosa mbalimbali ya faini waliohukumiwa nayo wafungwa hayo, kanisa lao limetoa
Sh milioni 6.8 kwa ajili ya kulipia faini hizo.
Awali Rwakatare
kupitia kanisa lake, aliwalipia wafungwa 78 katika magereza matatu ya Keko,
Segerea na Ukonga ya jijini Dar es Salaam na kuachiwa huru baada ya
kulipa faini ya Sh milioni 25 zilizochangwa na waumini wa kanisa hilo.
0 Comments