LIGI YA WANAWAKE KUANZA NOVEMBA 2



LIGI ya Taifa ya Wanawake Tanzania Bara itaanza Novemba 1, 2016 kama ilivyopangwa awali kwa kushirikisha timu 12 zilizopangwa kwenye makundi mawili yenye majina ya ‘A’ na ‘B’. Kila kundi lina timu sita.

Timu za kundi A lina timu za Viva Queens ya Mtwara, Fair Play ya Tanga, Mlandizi Queens ya Pwani pamoja na Mburahati Queens, Evergreen Queens na JKT Queens za Dar es Salaam wakati kundi B zimo Marsh Academy ya Mwanza, Baobab Queens ya Dodoma, MajengoWOMEN ya Singida, Sisters FC ya Kigoma, Kagera Queens ya Kagera na Panama FC ya Iringa.
Mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo utachukua takribani wiki tatu kwa makundi yote yaani hadi Novemba 20, mwaka huu na mzunguko wa pili utaanza Januari 4, 2017 hadi Februari mosi, mwakani.

Michezo ya kwanza kwa kundi A itakuwa ni kati ya Viva Queens na Mburahati Queens utakaofanyika Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara; wakati Fair Play itacheza na Evergreen ya Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga ilhali JKT Queens ya Dar es Salaam itakuwa wenyeji wa Mlandizi ya Pwani kwenye Uwanja wa Karume, Ilala jijini Dar es Salaam.

Kwa upande wa Kundi B michezo ya kwanza itakuwa ni kati ya Marsh Academy ya Mwanza itayoonyeshana kazi na MajengoWOMEN FC ya Singida kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza wakati Sister ya Kigoma itakuwa mwenyeji wa Panama ya Iringa kwenye Uwanja wa Tanganyika mjini Kigoma ilihali Kagera Queens itakuwa mgeni wa Baobab ya Dodoma kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini humo.
Ligi hiyo inakwenda kuanza ikiwa na mdhamini mmoja tu ambaye Kituo cha Azam Tv ambacho kitaonyesha michezo yote bure kupitia king’amuzi chake cha Azam.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), linatangaza kuwa kungali na fursa ya kudhamini ligi hiyo kutoka kwa watu binafsi na kampuni mbalimbali ambazo zitapata kutangazika wakati mechi za ligi hiyo zikiendelea.

Hii ni mara ya kwanza kwa Tanzania kuandaa ligi hiyo kwa upande wa wanawake ambako si tu kwamba itakuza kiwango cha soka kwa wanawake nchini bali inatarajiwa kuleta hamasa mpya katika mapenzi ya mpira wa miguu.


Pia benchi la ufundi la timu ya taifa kuweza kugundua vipaji vipya vitakavyojumuishwa kwneye timu ya taifa ambayo mwakani itaingia kwenye programu ya kuwania kucheza fainali za Kombe la Dunia kwa wanawake kutoka kanda ya Afrika. Fainali za Kombe la Dunia kwa wanawake zitafanyika mwaka 2019 huko Ufaransa.

Tuandikie Maoni Yako Hapa

Post a Comment

0 Comments