Mabingwa wapya wa Kombe la Chalenji la CECAFA, timu ya taifa ya wanawake ya Tanzania Bara maarufu kwa jina la Kilimanjaro Queens, inatarajiwa kurejea jijini Dar es Salaam kesho Septemba 22, 2016 saa 7.00 mchana kwa ndege ya FastJet ikitokea Mwanza.
Mara baada ya kutua, itakwenda moja kwa moja kwenye Hoteli ya Coartyard iliyoko Sea View, Upanga jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kupata chakula cha mchana ambako watakuwako viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na wale wa Serikali akiwamo Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mheshimiwa Nape Nnauye ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mtama mkoani Lindi.
Timu hiyo leo Septemba 21, 2016 ilitua Kagera ambako imetumia siku ya leo kuwafariji wahanga wa tetemeko la ardhi.
Itakumbukwa kwamba kabla ya kwenda Jinja, Uganda ambako ilivuna ubingwa huo katika fainali zilizofanyika jana kwa kuilaza Kenya katika fainali zilizofanyika Uwanja wa Njeru, Kilimanjaro Queens iliweka kambi mjini Bukoba ambako ilicheza mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Burundi na kushinda mabao 3-0 Septemba 8, mwaka kwenye Uwanja wa Kaitaba.
Kilimanjaro Queens inatarudi Kagera kusema: “Ahsante” kwa wenyeji akiwamo Mkuu wa Mkoa, Brigedia Jenerali Mstafu Salum Kijuu aliyewakabidhi bendera kabla ya safari, lakini pia kuwapa pole Wahanga wa janga la Tetemeko la Ardhi wakazi lililotokea katika mikoa huo na mikoa jirani ya Kanda ya Ziwa na nchi jirani. Mikoa ambayo iliathirika zaidi ni Kagera na Mwanza kadhalika nchi jirani za Uganda na Rwanda.
Mara baada ya kuwapa pole, timu hiyo itasafiri kutoka Kagera kwa usafiri wa anga ambako taratibu za safari hiyo zitatangazwa na TFF hapo kesho ambako wananachi watapata fursa ya kuipokea na kuishangilia timu hiyo inayonolewa na Kocha Sebastina Nkoma akisaidiuwa na Edna Lema wakiwa chini ya Mwenyekiti wa soka la wanawake, Amina Karuma.
0 Comments