Na Mwandishi Wetu – Singida
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Halima
Dendego, ametoa wito kwa wananchi wote wa mkoa huo kushirikiana na Serikali ya
Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.
Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kulinda na kutunza miundombinu ya shule mpya
zilizojengwa kwa lengo la kuinua kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi.
Akizungumza wakati wa kufanya tathmini
ya hali ya elimu mkoani Singida, Mhe. Dendego alisema kuwa juhudi kubwa
zimefanyika katika sekta ya elimu, ikiwemo ujenzi wa shule mpya, ili kutoa
fursa kwa wanafunzi kusoma katika mazingira bora na rafiki kwa ujifunzaji.
“Mkoa wetu umejipanga kuimarisha sekta
ya elimu kupitia maboresho makubwa yanayofanywa na Serikali. Tunahitaji
ushirikiano wa wananchi kuhakikisha miundombinu hii inadumu na kuwanufaisha vizazi
vya sasa na vijavyo,” alisema Dendego.
Kwa mujibu wa Mhe. Dendego, jumla ya
shule 30 za kata zimejengwa kupitia Mradi wa Kuimarisha Ubora wa Elimu ya
Sekondari (SEQUIP). Aidha, shule mpya ya wasichana ya Solya imejengwa katika
Wilaya ya Manyoni, huku shule mbili za amali – Kitukutu (Iramba) na Unyambwa
(Singida Manispaa) – zikikamilika na kuanza kutoa huduma kwa wanafunzi.
Amesisitiza kuwa wananchi wanapaswa
kuwa walinzi wa miundombinu hiyo kwa kuhakikisha inatunzwa ipasavyo na kutumika
kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuinua ubora wa elimu kwa ujumla.
0 Comments