WAFUGAJI SINGIDA WAOMBA SERIKALI IWAWEZESHE VIJANA KUJIAJIRI

 


Bi Catherine Kilongo Mfugaji wa kuku na Samaki akielezea na kuonesha aina ya kuu anaofuga.


 

  Bi Sianeli Lyimo mfugaji wa Samaki akielezea manufaa ya ufugaji wa samaki kitaalamu.


SINGIDA

Wafugaji kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Singida wameiomba serikali kuweka mkazo katika kuwawezesha vijana waliomaliza masomo yao ili waweze kujiajiri kupitia shughuli za ufugaji badala ya kusubiri ajira za ofisini.

Wito huo umetolewa na Bi. Catherine Kilongo, mkazi wa Kijiji cha Mtinko, ambaye ni mstaafu anayeendesha shughuli za ufugaji wa kuku na samaki. Bi. Kilongo amesema kuwa baada ya kustaafu aliingia rasmi kwenye sekta ya ufugaji na amekuwa akipata mafanikio makubwa ambayo aliwahi kuyakosa alipokuwa kwenye ajira ya kawaida.

“Shughuli za ufugaji zinalipa sana, kuliko hata ajira ya ofisini. Serikali iwasaidie vijana kwa elimu na mitaji ili nao wajiajiri,” amesema Bi. Kilongo.

Kwa upande wake, Bi. Sianeli Lyimo ambaye ni mfugaji wa samaki na aliyewahi kuwa muuguzi (Nesi) katika kituo cha afya ndani ya halmashauri hiyo, amesema aliamua kuacha kazi ya ajira rasmi baada ya kupata mafunzo ya ufugaji wa samaki. Kwa sasa, anajitegemea kupitia mradi wake wa ufugaji na amekuwa mfano kwa vijana wengine.

“Vijana wasisubiri ajira, waanze miradi yao. Ufugaji unalipa kama ukiamua kwa dhati,” amesema Sianeli.

Wafugaji hao wamesisitiza kuwa kwa mazingira ya Wilaya ya Singida, ambayo yanafaa kwa shughuli za ufugaji wa aina mbalimbali, serikali ina wajibu wa kuongeza juhudi katika kutoa mafunzo na mitaji kwa vijana ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kupunguza tatizo la ajira

Tuandikie Maoni Yako Hapa

Post a Comment

0 Comments