JESHI LA ZIMAMOTO SINGIDA LATOA ELIMU YA NISHATI SAFI NA TAHADHARI DHIDI YA MOTO

 


Kaimu kamanda wa jeshi la Zimamoto mkoa Singida ,Mrakibu Devota Bigawa akiwa ofisini kwake.

SINGIDA

Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Singida limeendelea na jitihada zake za kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi ya nishati safi, likilenga kuhamasisha utunzaji wa mazingira na kupunguza hatari ya majanga ya moto katika jamii.

Kaimu Kamanda wa Jeshi hilo, Mrakibu Debora Bigawa, amesema kuwa elimu hiyo inatolewa kama sehemu ya mikakati ya kuzuia majanga na kuhakikisha wananchi wanajua namna bora ya kutumia nishati salama majumbani mwao.

“Tunaendelea kuelimisha jamii kuhusu matumizi ya nishati safi kama gesi na majiko bora, sambamba na mbinu za kujikinga dhidi ya moto,” amesema Mrakibu Bigawa.

Aidha, amesema hadi sasa hakujatokea matukio makubwa ya moto mkoani Singida, isipokuwa tukio moja dogo lililoripotiwa hivi karibuni. Hata hivyo, amewataka wananchi kuendelea kuwa waangalifu na kuchukua tahadhari mapema.

“Usalama ni jukumu la kila mmoja wetu. Tunawashauri wananchi wahakikishe wana vifaa vya kuzimia moto majumbani na mahali pa kazi, na wawe na uelewa wa hatua za kuchukua pale majanga yanapotokea,” ameongeza.

Jeshi hilo limeeleza kuwa litazidi kushirikiana na jamii kupitia kampeni na warsha mbalimbali ili kuhakikisha elimu ya kinga dhidi ya moto inawafikia watu wengi zaidi, hasa vijijini ambako uelewa bado ni mdogo.

 Endelea kufuatilia ukurasa wetu kwa taarifa zaidi kuhusu usalama wa moto na matumizi ya nishati safi.


Tuandikie Maoni Yako Hapa

Post a Comment

0 Comments