MIAKA 6 YA MAFANIKIO YA MRADI WA USTAWI WA PUNDA SINGIDA





 Na Cales Katemana

SINGIDA:

Baada ya utekelezaji wa mafanikio wa miaka sita ya Mradi wa Ustawi wa Mnyama Punda, Shirika la INADES Formation Tanzania limetangaza mpango mpya wa kupanua huduma na elimu ya ustawi wa mnyama huyo kwa kata zote za Wilaya ya Singida.

Mradi huo, ambao ulilenga kuboresha hali ya maisha ya wanyama kazi hususan punda, ulianza kutekelezwa katika kata tatu pekee za Ghata, Endeshi, na Kinyamwenda, lakini kutokana na mafanikio yaliyopatikana, sasa unatarajiwa kuwafikia wafugaji katika maeneo mengine zaidi ya wilaya hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa INADES Formation Tanzania, Bi. Jaqueline Nicodemus, alisema:

“Tumeshuhudia mabadiliko makubwa katika maeneo tuliyofanyia kazi. Wananchi wamepokea elimu vizuri na kuna uelewa mkubwa juu ya haki, huduma na ustawi wa mnyama punda. Hii imetupa nguvu ya kupanua mradi huu zaidi.”

Kwa upande wake, Afisa Mradi wa Ustawi wa Mnyama Punda, Bw. George Farles, alibainisha kuwa jamii imeanza kuona thamani ya mnyama punda, na wameanza kubadilisha mitazamo yao kuhusu namna ya kumtunza.

“Katika miaka sita ya mradi, tumeshuhudia ongezeko la matumizi bora ya punda, upatikanaji wa huduma za matibabu na matumizi sahihi ya vifaa vya kazi kwa punda,” alisema Bw. Farles.

Aidha, Daktari wa Mifugo kutoka INADES, Dkt. Charles Lucas, alieleza kuwa shirika hilo limekuwa likitoa mafunzo ya kitabibu kwa maafisa mifugo waliopo kwenye kata husika, jambo ambalo limechangia kwa kiasi kikubwa kuboresha afya na ustawi wa punda.

“Kupitia mafunzo haya, tumeongeza uwezo wa wataalamu wa mifugo katika kutambua na kutibu magonjwa ya punda. Pia tumetoa elimu juu ya lishe, makazi, na matumizi ya vifaa visivyomdhuru mnyama,” alisema Dkt. Lucas.

Mradi huu wa INADES Formation Tanzania unatajwa kuwa mfano wa kuigwa katika kuboresha maisha ya wanyama kazi, ambao huchangia kwa kiasi kikubwa katika shughuli za usafirishaji wa mizigo na huduma nyingine vijijini.

Tuandikie Maoni Yako Hapa

Post a Comment

0 Comments