Hekima Chengula Mwakilishi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu akitoa Taaarifa fupi na Maelekezo.
Na Mwandishi wetu.
Maafisa Viungo wa Mikoa Tanzania Bara wametakiwa kukamilisha na kuwasilisha taarifa za utekelezaji wa Ilani ya CCM kupitia Mfumo wa Dashboard ifikapo Julai 15, 2024.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Tawala za Mikoa Ofisi ya Rais TAMISEMI Bi. Beatrice Kimoleta wakati akifunga mafunzo na kikao kazi kwa Maafisa Viungo wa Mikoa Tanzania Bara tarehe 7 Juni, 2024 katika Manispaa ya Singida mkoani Singida ambapo aliwaagiza Maafisa hao kukamilisha taarifa za Ilani kwa usahihi, uhalisia, kuziingiza kwenye mfumo na kuziwasilisha kupitia Mfumo wa Dashboard kwa wakati.
“kwa kuwa kipindi hiki tunaendelea na maandalizi ya mpango kazi na taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa mwaka 2024, nitumie fursa hii adhimu kusisitiza kuwa taarifa za utekelezaji wa Ilani za Mikoa kipindi cha Januari hadi Juni, 2024 zikamilishwe na kuwasilishwa kupitia mfumo wa Dashboard ifikapo tarehe 15 Julai, 2024” alisema Bi. Kimoleta.
Aidha, amewataka Maafisa hao kahakikisha kuwa mikoa yao inaandaa vikao kazi vya kupitia vishiria vilivyopo na vinavyotakiwa kutekelezwa na Halmashauri ili kuwa na picha ya pamoja ya taarifa zinazotakiwa kuingizwa katika mfumo vyenye taarifa sahihi na uhalisia, kazi ya kuingiza kwenye mfumo viashiria vilivyohuishwa na kukubaliwa katika kikao na mpango kazi wa utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa mwaka 2024 vinakamilika ifikapo Juni 14, 2024 pamoja na kuzingatia ratiba za uwasilishaji wa mpango na taarifa za utekelezaji wa Ilani ya CCM ili kutoa nafasi kwa ngazi za juu kuchambua, kuhakiki na kuandaa taarifa jumuishi kwa umakini na kuwasilisha kwa kuzingatia mahitaji ya viongozi.
Akitoa maelezo ya awali kabla ya hotuba ya mgeni rasmi Bw. Hekima Chengula Mwakilishi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu alisema Ofisi yake ndiyo iliyopewa jukumu la kuratibu uandishi wa Ilani ya CCM Kitaifa ikishirikiana na Wadau wengine ikiwemo Ofisi ya Rais TAMISEMI na Mikoa lakini pia ameahidi kuifanyia kazi changamoto ya Mfumo wa Ilani kwa niaba ya ofisi yake lakini pia anayo matarajio ya kuona viashiria vya Ilani vimeingizwa kwenye Mfumo na Mpango kazi unaotekelezeka umeandaliwa na Mikoa.
Akitoa neno la utangulizi kabla ya hotuba ya mgeni rasmi Bw. Johnson Nyingi Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Uratibu wa Shughuli za Serikali Ofisi ya Rais TAMISEMI amesema mafunzo hayo yameleta tija kwa washiriki wote kwani uelewa wao umeongezeka lakini pia wamekubaliana aina ya viashiria watakavyovitumia katika Sekta zote na hivyo matarajio ni kuwa uandaaji wa taarifa zote za Ilani ya CCM zitakuwa na muundo ulio sawa bila kuwa na utofauti kama hapo awali.
Naye Mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa wa Singida Romwaid Mwendi Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Mipango na Uratibu. alisema Ofisi ya Rais TAMISEMI itarajie kupokea taarifa sahihi za Ilani ya CCM zilizo bora lakini pia aliwaomba wataalam wa Mfumo kufanya maboresho ya Mfumo wa Ilani ili wanaoandaa taarifa waweze kuhariri pindi wanapotaka kufanya maboresho ya taarifa zao.
Akitoa neno la shukrani bi. Susana Ndunguru Mwenyekiti wa Maafisa Viungo Tanzania Bara ameahidi kuandaa taarifa sahihi na kuzitoa kwa wakati na ametoa rai kwa Ofisi ya Waziri Mkuu kuondoa taarifa ambazo ziliwekwa kwenye mfumo wa Ilani hapo awali ambazo zinamakosa waziondoe kwani Mfumo huo hauruhusu kufuta taarifa ambazo tayari zimehifadhiwa.
Mafunzo hayo ya siku
nne yaliyoandaliwa kati ya Ofisi ya Rais TAMISEMI na Ofisi ya Waziri Mkuu yana
lengo la kuwajengea uwezo Maafisa Viungo wa Mikoa kupitia mpango kazi wa
utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020 ili kuandaa mpango
kazi wa mwaka 2024 yakihusisha Maafisa Viungo wa Mikoa 26, Maafisa Viungo wa
Halmashauri za Mkoa wa Dar es Salaam, Wataalam kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI na
Wataalam kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu.
0 Comments