SHIRIKA la “Afrika Muslim Agency” (AMA) linalomiliki shirika la
misaada la Direct Aid kutoka nchini Kuwait limefungua kisima cha maji cha
msikiti wa Masjid Khadri ya Ititi chenye urefu wa mita 94 kilichogharimu
shirika sh. 35 milioni, katika kijiji cha Mnang’ana kitakachotumika kwa
wanakijiji 4,100 kwa kupata maji safi na salama.
Akizungumza na wananchi wa kijiji hicho juzi kwa lugha ya
kiarabu Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo Kanda ya Afrika Sheik Mohamed Rabba
ameahidi kutoa misaada kwa wananchi wa Mkoa wa Singida ili wapate maji
safi na salama ya kunywa kwa kuwachimbia visima virefu na vifupi kama moja ya
imani kwa Mungu aliye muumba na mtume wake Muhammad.
Sheikh Rabba amesema katika ufunguzi huo wa kisima kuwa
mradi huo wa maji ulikuja rasmi kwa ajili ya Msikiti Mkuu wa Ititi lakini
wananchi wa kijiji cha Mnang’ana wameutaka uenee kijiji chote na shirika
limekubali wito huo kama moja ya malengo yake katoka nchi yake.
Sheikh Rabba amesema nchi yake Kuwait kwa kupitia Balozi wake
nchini Jassem Al- Najem imejikita kuboresha maji, afya, elimu, barabara na
umeme vijijini kwa wananchi wa Tanzania na sasa mkoa wa Singida.
Aidha Injinia wa shirika hilo mkoani Singida Adam Said Mussa
amesema shirika lake limeamua kuweka mikakati ya nguvu kwa wananchi mkoani
Singida ili waweze kwenda vizuri na kasi ya serikali kwa kuwachimbia visima vya
maji vingi mahali walipo kwa ukaribu zaidi kila mita 400 kuwa na kisima cha
maji salama ya kunywa.
Mussa amesema shirika lake limejikita kuchimba visima kwa
kutumia mitambo ya kisasa kutoka Kuwait ili kuwawezesha wananchi kupata maji
safi na salama ya kutosha kwenye maeneo yao ili waweze kupata nafasi ya kufanya
mambo mengine ya kuwaletea maendeleo.
Naye kwa upande wake msimamizi wa mradi huo Singida ustaadhi
Juma Rashidi Nkindwa amesema ujenzi wa mradi huo ulianza mwezi June 2017 hadi
Julai ukiwa umepewa namba 30147 una mantanki mawili makubwa na umegharimu sh.
35 milioni na mafundi wa uchimbaji wamebainisha maji yalipo kwenye kisima hicho
yanatosha kuwapatia maji wanakijiji mwa miaka 25.
Diwani wa Kata ya Sepuka Yusufu Missanga amewataka wanakijiji
kutunza mradi huo vizuri ili utumike kwa muda mrefu kuendeza kilimo cha
umwagiliaji na amewashukuru wafadhili kwa kuamua kutoa msaada huo wa maji kwa
msikiti wa Masjid Khadriya na kwa wananchi wa kijiji cha Mnang’ana na
hiyo itahamasisha wananchi wenyewe kujiletea maendeleo.
1 Comments
Assalamu a'laikum warahmatullah wabarakatuh vipi Hali .
ReplyDeleteNaitwa Albatuli, kutoka SINGIDA.
Tunauhitajio WA kuchimbiwa kisima kwenye eneo letu lililopo ititi, Ili tuweze kufanikisha shughuli yetu ya ujenzi WA msikiti.
Kwa mawasiliano 0785048710