MBUNGE YAGI KIARATU AZUNGUMZA NA WAZEE WA SINGIDA, ASIKILIZA KERO ZA

 





SINGIDA

Mbunge wa Jimbo la Singida Mjini, Mhe. Yagi Kiaratu, amezungumza na wazee wa Manispaa ya Singida katika mkutano maalum uliofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) mjini Singida.

Mkutano huo ulifunguliwa rasmi na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Singida, Bi. Lucia Mwiru, na kuhudhuriwa na wazee maarufu kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa huo, viongozi wa dini, wastaafu waliowahi kushika nyadhifa tofauti za uongozi katika mkoa wa Singida, pamoja na wataalamu kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Singida.

Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Yagi Kiaratu alipata fursa ya kusikiliza kero na changamoto mbalimbali zilizowasilishwa na wazee hao, ambapo alijibu maswali yao papo kwa papo na kutoa ufafanuzi juu ya masuala yanayohusu maendeleo ya jimbo hilo. Aidha, alipokea salamu za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zilizotolewa na wazee mbalimbali waliohudhuria mkutano huo.

Mbunge huyo aliwataka wazee kuendelea kuwa nguzo ya amani kwa kushirikiana kwa karibu na vijana wao, ili kuepusha uvunjifu wa amani ulioshuhudiwa hivi karibuni katika baadhi ya kata na mikoa nchini. Alisisitiza kuwa wazee wana nafasi kubwa katika kutoa malezi, ushauri na maelekezo sahihi kwa vijana ili kudumisha mshikamano na utulivu wa jamii.

Pia, Mhe. Yagi Kiaratu alitumia fursa hiyo kuwashukuru wananchi wa Singida Mjini, hususan wazee, kwa kumuamini na kumchagua kuwa Mbunge wa jimbo hilo katika Uchaguzi Mkuu uliopita, akiahidi kuendelea kushirikiana nao katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya Singida.

Mkutano huo ulimalizika kwa wazee kupongeza hatua ya Mbunge wao kukutana nao ana kwa ana na kusikiliza maoni yao, wakieleza matumaini makubwa ya kuendelea kushirikiana na uongozi wa serikali kwa maendeleo na ustawi wa jamii ya Singida.

Tuandikie Maoni Yako Hapa

Post a Comment

0 Comments