DKT. MWIGULU AKAGUA MIRADI YA MAJI RUVU CHINI, SERIKALI YAJIPANGA KUKABILI UPUNGUFU WA MAJI

Waziri Mkuu Dkt Mwigulu Nchemba akiongea na watumishi baada ya kukagua mradi huo.






PWANI 

Na Mwandishi wetu 

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, leo Desemba 29, 2025, amefanya ziara ya ukaguzi katika eneo la Ruvu Chini, mkoani Pwani, kukagua hali ya uzalishaji na usambazaji wa maji.

Ziara hiyo imelenga kujionea kwa karibu utekelezaji wa miradi ya maji pamoja na hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kukabiliana na changamoto ya upungufu wa maji inayochangiwa na mabadiliko ya tabia ya nchi.

Akizungumza baada ya ukaguzi huo, Dkt. Mwigulu amesema kuwa Serikali ilianza mapema kutambua changamoto ya upatikanaji wa maji na hivyo kuanza kutekeleza miradi mikubwa ya maji katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Amesisitiza kuwa mipango hiyo haikuanza kwa bahati mbaya, bali ilitokana na tathmini ya kina iliyofanywa na Serikali kuhusu athari za mabadiliko ya tabia ya nchi, ambapo juhudi kubwa zimeelekezwa katika ujenzi wa miradi ya kimkakati inayolenga kutoa suluhisho la kudumu kwa wananchi.

“Mipango hii ya ujenzi wa miradi ya maji ilianza muda mrefu. Serikali iliona changamoto mapema na kuanza kutafuta majawabu yake miaka mitatu iliyopita kwa kujenga miradi mikubwa itakayotoa matokeo chanya kwa wananchi,” amesema Dkt. Mwigulu.

Serikali imeendelea kusisitiza dhamira yake ya kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama kwa uhakika, huku miradi kama ya Ruvu Chini ikitarajiwa kuongeza upatikanaji wa maji kwa maeneo ya Pwani na Dar es Salaam kwa ujumla.

Tuandikie Maoni Yako Hapa

Post a Comment

0 Comments