TANZANIA YAPONGEZWA KWA UTEKELEZAJI WA MKATABA WA UMOJA WA MATAIFA DHIDI YA RUSHWA

 



Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru Bw Crispin Francis Chalamila akitoa taarifa ya Tanzania 

Doha Qatar

Pongezi hizo zimetolewa hivi karibuni wakati Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Bw. Crispin Francis Chalamila alipotoa taarifa ya Tanzania kuhusu utekelezaji wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa dhidi ya Rushwa kwenye Mkutano Mkuu wa 11 wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa dhidi ya Rushwa unaoendelea jijini Doha, Qatar. Mkurugenzi Mkuu Chalamila anaongoza ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano Mkuu huo ulioanza tarehe 15 hadi 19 Desemba, 2025 jijini Doha, Qatar.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mkataba, Bw. Chalamila alisema “Rushwa inaendelea kuleta changamoto katika mataifa mmbalimbali kwa kudhoofisha utawala, kudorora kwa ukuaji wa uchumi, kuongezeka kwa umaskini, kukiukwaji wa haki za binadamu, huduma za umma zisizo na tija, kudhoofisha taasisi na maendeleo potofu.”

Aidha, Tanzania imepongezwa kwa kuimarisha mifumo ya uzuiaji rushwa kupitia utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa dhidi na Rushwa na Mpango wa Utekelezaji (NACSAP IV), kuboresha mifumo ya manunuzi ya Umma kupitia Sheria ya Ununuzi ya Umma ya mwaka 2023, kuimarisha utaratibu urejeshaji wa mali zilizpopatikana kwa njia za uhalifu ikiwemo rushwa kupitia Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, na kuimarisha taasisi simamizi ikiwemo TAKUKURU, Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu, Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Alieleza kuwa, kufuatia kukamilika kwa Mzunguko wa Mapitio ya Kwanza wa Tanzania Kupimwa ilivyotekeleza Mkataba wa UNCAC (First Review Cycle), uliofanywa na nchi za Austria na Msumbiji, Tanzania ilionekana kuwa imefanya mageuzi makubwa katika kuimarisha mfumo wa kitaifa wa kudhibiti uhalifu, utekelezaji wa sheria na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa.

Mkutano Mkuu wa 11 wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa dhidi ya Rushwa hufanyika kila baada ya miaka miwili ukiwakutanisha wakuu wa taasisi simamizi dhidi ya rushwa, watunga sera, viongozi wa kisiasa, asasi za kiraia, asasi zisizo za kiserikali, pamoja na wadau wa maendeleo. Mkutano huu unaoendelea jijini Doha umekutanisha washiriki zaidi ya 3000 kutoka mataifa mbalimbali chini kauli mbiu inayosema “Shaping Tomorrow’s Integrity.”

 

Tuandikie Maoni Yako Hapa

Post a Comment

0 Comments