Waziri Mkuu Dkt Mwigulu Nchemba ameanza ziara Mkoani Singida akiwa Manyoni amekagua Mradi wa Bandari Kavu na Kutoa maelekezo juu ya Mkandarasi.
Na Cales Katemana
Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, ameanza
rasmi ziara yake ya pili mkoani Singida, ikiwa ni mwendelezo wa ukaguzi wa miradi ya
kimkakati inayotekelezwa katika mkoa huo. Ziara hii inafuatia ukaguzi
alioufanya katika Hospitali ya Mkoa wa Singida hivi karibuni.
Katika siku ya
pili ya ziara hiyo, Dkt. Nchemba ametembelea kwa mara ya kwanza mradi wa
ujenzi wa Bandari Kavu (Dry Port) wilayani Manyoni, mradi ambao umekuwa
ukisuasua kwa muda mrefu.
Akiwa eneo la
mradi, Waziri Mkuu alielezwa kuwa ujenzi wa bandari hiyo umesimama kwa zaidi
ya miaka nane, baada ya mkandarasi kushindwa kukamilisha mradi na kudaiwa
kufilisika.
Mradi huo,
unaojulikana kama Construction of One Stop Inspection Station (OSIS) – Lot 1,
ulianza kutekelezwa Mei 2017 na ulipaswa kukamilika Novemba 2018. Mkandarasi
aliyekuwa amepewa jukumu la ujenzi ni Impress di Construczioni Ing. E,
ambapo thamani ya mradi inakadiriwa kufikia Euro 9,537,607.90, sawa na Shilingi
za Tanzania 26,823,568,457.96.
Katika
kuhakikisha nidhamu na uwajibikaji unazingatiwa, Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu
ameagiza mamlaka husika kukamata pasipoti ya mkandarasi huyo, hadi pale
atakapokamilisha mradi au kuukabidhi rasmi kwa serikali ili hatua nyingine
ziendelee.
Aidha,
amesisitiza kuwa serikali haitavumilia miradi ya maendeleo kusimama kwa muda
mrefu, hasa ikizingatiwa umuhimu wake kwa wananchi na uchumi wa taifa.
“Hatutaacha
miradi kukaa miaka mingi bila kukamilika wakati wananchi wanahitaji huduma.
Lazima thamani ya fedha ionekane,” amesisitiza Dkt. Mwigulu.
Wakazi wa Manyoni
na Mkoa wa Singida kwa ujumla wamesema wana matumaini makubwa kuwa hatua
zilizochukuliwa na serikali zitafungua njia ya kukamilika kwa mradi huu muhimu,
ambao ukikamilika utarahisisha shughuli za usafirishaji, ukaguzi na biashara
katika ukanda wa kati.






0 Comments