(picha kutoka maktaba yetu)
Na Mwandishi wetu -(w) Ikungi
Watoto Waliozaliwa Wakiwa na Miezi Nane Wapatiwa Huduma Maalum za Joto
Mwanamke mmoja mkazi wa Kijiji cha Msungua, Kata ya Sepuka, Wilaya ya Ikungi mkoani Singida, Muridi Juma Masambai (37), amejifungua watoto watatu wakike katika Hospitali ya Rufaa ya Singida iliyoko Mandewa, nje kidogo ya mji wa Singida.
Muridi alihamishiwa hospitalini hapo kutoka Kituo cha Afya Sepuka baada ya wataalamu wa afya kushauri ajifungulie katika kituo hicho kikubwa kutokana na hali ya ujauzito na afya yake.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Subira Iddi, muuguzi aliyemhudumia mama huyo, Muridi alijifungua salama tarehe 17 Oktoba 2025, lakini watoto hao waliwekwa kwenye mashine maalum za joto kwa kuwa walizaliwa wakiwa na umri wa miezi nane na wiki mbili.
Akizungumza na mwandishi wa habari, Yahaya Msafiri, baba wa watoto hao, alisema kuwa mtoto wa tatu alifariki dunia baada ya kuishi siku 12 tu tangu kuzaliwa akiwa na uzito wa kilo 1.6.
Watoto waliobaki wana uzito wa kilo 1.9 na 1.8.
Yahaya alieleza kuwa mke wake alipata changamoto ya upungufu wa damu na maziwa, lakini alisaidiwa damu na watu wanane hospitalini hapo.
Bwana Yahaya alimshukuru Mungu kwa zawadi ya watoto watatu kwa mara moja, lakini alionyesha huzuni kwa kumpoteza mmoja wao.
Aidha, alitoa ombi kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, taasisi za kidini, watu binafsi na wadau mbalimbali kumsaidia katika malezi ya watoto waliobaki, kwani hana uwezo wa kifedha.
Kwa mujibu wa wazazi hao, mtoto wa kwanza amepewa jina Rais Dkt. Samia, akiwa na uzito wa kilo 1.9, na wa pili amepewa jina Ruth, ambaye ni mama wa Mbunge Elibariki Kingu, kutokana na heshima kwa viongozi hao waliokuwa kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
mari Bayyu, Mwenyekiti wa Kijiji cha Msungua, aliwatembelea wazazi hao na kuwapa pole pamoja na pongezi kwa tukio hilo la furaha.
Alisema majina waliyochagua yanawakilisha viongozi mashuhuri na jasiri wa taifa, akiahidi kutoa msaada wa hali na mali kwa familia hiyo.
Aidha, wananchi wa kijiji hicho waliungana kutoa pongezi kwa wazazi hao na kuomba wadau mbalimbali wawasaidie kutokana na hali yao ya kifedha kuwa duni.




0 Comments