TAMASHA LA “SINGIDA PAMOJA DANCING” LAMWAGA BURUDANI, RC DENDEGO ATOA WITO KWA VIJANA

 


Mkuu wa Mkoa wa Singida akiongea katika uzinduzi wa Tamasha la SINGIDA PAMOJA DANCING.


                              




SINGIDA

Na Cales Katemana

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Halima Dendego, amewataka vijana wenye vipaji mbalimbali mkoani humo kujitokeza kwa wingi kuonesha vipaji vyao ili serikali iweze kuvibaini na kuvikuza kupitia wataalamu waliopo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa tamasha kubwa la "Singida Pamoja Dancing" lililofanyika katika viwanja vya Bombadia mjini Singida, Mhe. Dendego alisema kuwa sanaa kwa sasa ni ajira yenye kipato kinachoweza kubadilisha maisha ya vijana wengi.

Alitolea mfano nyota wa kimataifa waliotokea Singida akiwemo mwanariadha Felix Simbu na mchezaji wa timu ya taifa ya wanawake, Twiga Stars, anayekipiga soka la kulipwa Aisha Msaka, akisema kuwa ni mifano halisi ya namna vipaji vinavyoweza kumuinua kijana na taifa kwa ujumla.

Akijibu risala ya washiriki na waandaaji wa tamasha hilo, Mkuu wa Mkoa alisema ameyapokea maombi yao na atayafanyia kazi mara moja. Pia aliwataka vijana kutojihusisha na vitendo vya uvunjifu wa amani, badala yake wawe wabunifu na wachapa kazi kwa maendeleo yao na ya mkoa mzima.

Aidha, aliwahimiza vijana kujitokeza kwa wingi kushiriki katika uchaguzi utakaofanyika Oktoba 29, akisema ni fursa muhimu ya kuchagua viongozi watakaowawakilisha vyema.

Tamasha hilo lilihusisha vijana kutoka vyuo mbalimbali, shule za msingi na sekondari kutoka maeneo tofauti ya mkoa wa Singida. Pia lilipambwa na burudani mbalimbali zikiwemo michezo ya dansi, nyama choma, na mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Yanga na Silver Strikers ya Malawi, iliyotazamwa mubashara na mashabiki wa soka waliofurika uwanjani.



Tuandikie Maoni Yako Hapa

Post a Comment

0 Comments