Klabu ya Simba imekabidhiwa kitita cha shilingi milioni 100 na
wadhamini wake, kampuni ya SportPesa, kama zawadi ya pongezi baada ya
kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2017/18.
Kwa mujibu wa masharti ya mkataba walioingia na kampuni hiyo ya
bahati nasibu, mojawapo ya kipengele kinaeleza kutoa kiasi hicho cha fedha
endapo timu itafanikiwa kutwaa ubingwa wa ligi.
Hundi ya fedha hizo imetolewa leo na Mkurugenzi wa SportPesa
nchini, Abbas Tarimba, kupitia kikao kilichoitishwa mbele ya Waandishi wa
Habari katika ofisi za kampuni hiyo jijini Dar es Salaam.
Kwa ujumla klabu ya Simba inakuwa imejinyakulia kiasi cha
milioni 180 ukijumlisha na zile za ubingwa wa ligi ambazo hutolewa na Mdhamini
Mkuu, Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom.
Kampuni ya Vodacom itawakabidhi Simba fedha zao kiasi cha
milioni 80 mapema baada ya ubingwa wa ligi kumalizika.
Wakati huo huo Shirikisho
la Soka Barani Africa (CAF) limefanyia mabadiliko ratiba ya michuano ya Kombe
la Shirikisho pamoja na Ligi ya Mabingwa Afrika iliyokuwa ikifanyika kwa mwezi
Februari hadi Novemba.
Mabadiliko hayo yanaonesha kuwa ratiba ya michuano hiyo itakuwa
inafanyika mwezi Mei mpaka Agosti badala ya ilivyokuwa imezoeleka.
Imeelezwa sababu kubwa iliyopelekea kubadilishwa kwa ratiba hiyo
ni kuendana sambamba na michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UEFA
Champions League) ambayo huchezwa wakati ligi zinaendelea.
Kwa msimu ujao mashindano hayo yataanza mwezi Disemba mpaka Mei
ikiwa ni kabla ya mabadiliko tajwa hapo juu kuanza kutumika rasmi.
Uamuzi huo umekuja wakati klabu ya Simba hapa nchini ikiwa
tayari imeshakata tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuutwaa
ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu.
Wakati huo mwakilishi wa Kombe la Shirikisho Afrika bado
hajapatikana ambapo baada ya mchezo wa fainali ya Azam Sports Federation CUP
kati ya Singida United na Mtibwa Sugar ndiyo unaotarajiwa kupigwa siku kadhaa
zilizosalia utatoa rasmi timu itakayoshiriki.
0 Comments