Duru la Pili la Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara inatarajiwa kuanza kesho Jumamosi Desemba 17 kwa michezo
minne kabla ya michezo mingine minne kufanyika siku ya Jumapili Desemba 18,
mwaka huu.
Katika mechi za kesho, Mabingwa
watetezi wa taji hilo, Young Africans SC ya Dar es Salaam itakuwa mgeni wa JKT
Ruvu ya Pwani kwenye mchezo utakaofanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Licha ya kwamba mwenyeji wa
mchezo huo ni JKT Ruvu ambayo uwanja wake wa nyumbani mara nyingi huwa ni
Mabatini ulioko Mlandizi, lakini kwa mujibu wa Kanuni ya 6 (5) na (6) ya Ligi
Kuu Bara, mechi zake za nyumbani dhidi ya Simba, Young Africans na Azam FC,
hufanyika Uwanja wa Uhuru.
Michezo mingine ya kesho ni
Kagera Sugar kuwa mgeni wa Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya
wakati Ruvu Shooting ya Pwani itakuwa mwenyeji wa Mtibwa Sugar ya Morogoro
kwenye Uwanja wa Mabatini, Pwani ilihali Mwadui ya Shinyanga itaikaribisha Toto
Africans ya Mwanza kwenye Uwanja wa Mwadui Complex.
Jumapili, Desemba 18, mwaka huu
Mbao FC ya Mwanza itacheza na Stand United ya Shinyanga kwenye Uwanja wa CCM
Kirumba, Mwanza wakati Ndanda itakuwa mwenyeji wa Vinara wa Msimamo katika Ligi
Kuu ya Vodacom, Simba kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.
African Lyon ya Dar es Salaam
itaikaribisha Azam FC pia ya Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Uhuru jijijini siku
hiyo ya Jumapili wakati Majimaji ya Songea itakuwa Mbeya kucheza na Tanzania
Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine.
Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania, limetoa masharti kadhaa likitaka klabu za Ligi Kuu ya Vodacom
kufuata.
Masharti hayo, ni kwa klabu
kutumia makocha wenye sifa kwa mujibu wa kanuni ya 72 ya Ligi Kuu ya Vodacom.
Kwa mujibu wa Bodi ya Ligi Kuu ya Shirikisho la Mpira wa Tanzania (TFF) na kwa
mujibu wa kanuni hiyo, makocha wanaopaswa kukaa kwenye benchi la Ligi kuu kwa
msimu huu wasipungue sifa ya kuwa na leseni B ya CAF.
Pia kwa timu za Ligi Daraja la
Kwanza na Pili, masharti ni lazima makocha wawe na sifa za kuzinoa timu hizo
ambazo zimeanishwa kwenye kanuni za ligi husika.
Kadhalika, tunaagiza klabu
kutotumia wachezaji wa kigeni au makocha kama hawana vibali vya ukaazi na
kufanya kazi kutoka Idara ya Uhamiaji nchini iliyoko chini ya Wizara ya Mambo
ya Ndani.
0 Comments