TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI NA WATANZANIA WOTE.
Kutoka mezani kwangu Moses Joseph Machali, Tarehe: 21/11/2016
Napenda kuutaarifu umma wa Watanzania kupitia kwenu waandishi wa
habari kwamba ni jambo la ajabu na aibu kwa watu makini na wenye kuhitaji
mabadiliko ya kweli Kuacha kuunga Mkono juhudi zinazofanywa na serikali ya
awamu ya tano chini Uongozi wa Rais Dr. John Pombe Joseph Magufuli bila kusahau
utendaji makini wa Waziri Mkuu wake Mhe. Majaliwa Kasim Majaliwa (Mb) pamoja na
mawaziri mbalimbali wameonesha kutaka kufuata mwenendo wa Rais Magufuli na
Waziri Mkuu wake.
Mimi Moses Joseph Machali niliyefanya sana siasa za Upinzani
hapa nchini na niliyepiga kelele na kupinga siasa za kifisadi zilizoitawala
nchi hii; niliyepinga pia ufisadi uliokuwa umeitawala serikali huko nyuma kwa
nguvu na uwezo wangu wote nikishirikiana na wapinzani wenzangu, ninaamua
kujiunga na watu wanaonesha dhamira safi ya kuiendeleza nchi yetu Tanzania.
Watu wenye mwelekeo na dhamira ya kuijenga nchi yetu kwa maendeleo enedelevu ni
jamii ya akina Magufuli, Kasim Majaliwa, nk.
Mwaka mmoja wa Uongozi wa Rais Magufuli na baadhi ya wasaidizi
wake kupitia hatua mbalimbali zilizochukuliwa dhidi ya ufisadi uliokuwa
umeigubika nchi yetu, inatosha kabisa kwa mtu yeyote makini kufanya uamuzi wa
kumuunga mkono au kutokumuunga mkono Rais Magufuli.
Mimi nimechagua kumuunga Mkono Rais kwa vitendo, kwa sababu
ninaposoma Rekodi yangu ya enzi nikiwa Mbunge (Hansard) na kabla ya kuwa mbunge
ni kwamba nilipinga mnoo wizi na ufisadi wa kila aina; Nilipinga Matumizi ya
fedha serikalini yasiyo ya lazima na yasiyo na tija kwa taifa (Rejeeni hotuba
yangu ya Bajeti ya Wizara ya Uchukuzi, nikiwa Waziri Kivuli wa wizara hiyo ya
mwaka 2014/2015 na 2015/2016), vilevile bila kusahau hotuba zangu mbalimbali
Bungeni na nje ya Bunge.
Kwa kushirikiana na wapinzania wenzangu enzi hizo tulishauri na
kupinga ufisadi wa kila aina, tuliitaka serikali kufanya mambo yenye tija kwa
taifa na sasa kila mwenye macho anaona hatua zinazochukuliwa na serikali ya
awamu ya tano. Miradi kama ya Ujenzi wa Reli, Ununuzi wa ndege mbili na mipango
ya kununua ndege zaidi kama namna ya kulifufua shirikia la ATCL ni mambo
tuliyoyahitaji kuyaona wapinzani; sasa yanafanyika. Wale wenye dhamira ya dhati
ya kuona nchi yetu ikipiga hatua, kamwe hatuwezi kubeza mambo hayo bali
kuyaunga mkono.
Wale tuliosema na kupiga kelele kwamba Serikali ni dhaifu ktk
kuwachukulia hatua watu mbalimbali wenye dhamana serikalini walioonekana
kufanya vibaya serikalini ktk nafasi zao, leo tunaona kumekuwepo na kasi nzuri
ktk kuwachukulia hatua watu hao. Hata hivyo leo hii upinzani umepiteza mwelekeo
kwa sababu unapingana na kile ulichokihubiri nchini.
Agenda ya kupinga ufisadi siyo ya upinzani tena bali ya JPM na
CCM yake au yao. Wapinzani wamegeuka kuwa watu wanaokataa yale waliyoyasimamia
na kuyahubiri huko nyuma. Hakika huo siyo uungwana bali aina mpya ya ufisadi
nchini na usaliti kwa agenda zao.
Kama kweli sisi tumeokuwa wapinzani na tulioonesha kupinga kwa
nguvu zote ufisadi ulioiumiza nchi hii tulimaanisha yale tuliyoyahubiri na
kuwaaminisha watu basi tunao wajibu wa kuacha tabia ya kuwa vigeugeu kwa mambo
tuliyoyaamini na kuyahubiri. Kutofanya hivyo basi ni mwendelezo wa ufisadi kwa
maslahi binafsi.
Ni nani asiyeona kwamba serikali ya awamu ya tano inafanyia kazi
mambo mengi tuliyoyapigia kelele? Au tunajifanya kutokukubali ukweli unaoishi
kwa ule msingi wa upinzani wa Tanzania kwamba Tukimuunga mkono Mtawala kamwe
hatutapata kuaminiwa na wapiga kura nchini na hivyo tupinge tu hata kama ni
ukweli? Nadhani kinachofanyika ni mwendelezo wa kupinga hata mazuri ili
kutafuta fursa ya wapinzani kukubalika kisiasa zaidi hata kwa njia na mbinu
haramu kama kawaida ya siasa zilizo zoeleka hapa nchini kwa miaka mingi.
Taifa hili haliwezi kuendelea kwa kuwa na siasa za
kutokukubaliana na ukweli unaoishi. Kama dhamira ya kila mtanzania ikiwemo
wapinzani ni kuona nchi ina move basi hatuhitaji kuwa watu wa kupingapinga hata
yaliyo mema bali kuyaunga mkono yale yaliyo mema bila kujali yanafanywa na nani
bali msingi mzuri unapaswa kuwa ukweli kwa kila jambo.
Serikali ya awamu ya tano imeonesha njia ktk mambo mengi na
inastahili kuungwa mkono. Safari ni hatua na ninaamini kwamba hata yale
yanayoonekana kutokufanyiwa kazi ndani ya mwaka mmoja uliopita na ambayo
yalishindikana huko nyuma, bado yanaweza kuja kufanyiwa kazi huko mbeleni.
Serikali ya JPM imejitahidi sana tukilinganisha na huko tuliko toka. Uongozi
huu unafanana sana na ule wa akina Hayati EDAWARD MORINGE SOKOINE chini ya
hayati Baba wa Taifa Mwl Julius Kambarage Nyerere.
Daima ninaamini ktk yale ninayoyaamini pasipo kufungwa na ukada
bali kuangalia ukweli ni upi. Hata kelele wanazopiga baadhi ya watu kwamba
maisha yamekuwa magumu kwa sababu ya Magufuli ni propaganda tu kwa sababu
hakuna uhusiano wa maisha magumu na suala la KUDHIBITI wapiga dili wa fedha na
mali za umma bali tukubali kwamba wapiga dili waliozoea kupiga dili na
kuziingiza fedha walizopiga ktk mzunguko kwamba siyo jambo la msingi ktk
kujenga uchumi imara.
Uchumi imara hauwezi kujengwa kwa kuruhusu ubadhirifu wa fedha
na mali za umma au hata za mtu mmoja mmoja. Kinachoonekana hivi sasa ni kama
nchi inasukwa upya na hivyo tuwaunge mkono viongozi wa serikali ya awamu ya
tano kwa mema wanayoyafanya na kuwashauri kurekebisha ktk yale ambayo hayajakaa
vizuri. Tuachane na siasa nyepesi za kutaka kuona kwamba mazuri ni yale yanayofanywa
na wapinzani huku mambo hayohayo yakifanywa na CCM yaonekane hayafai na kutajwa
kuwa ni ya hovyo. CCM ya JPM siyo ile ya 2015 kurudi nyuma kidogo. Hii ni
tofauti na ninaiunga mkono.
Hivyo basi leo Tarehe 21/11/2016 ninatangaza rasmi kwamba ninajiunga
na timu JPM kwa maslahi ya taifa kwa kuwa sioni sababu ya kupingana na yale
niliyoyapigania na itakuwa ni sawa na mtu kupigana na kivuli chake mwenyewe.
Kwaherini Upinzani nimeamua kuanza siasa mpya za masuala yale niliyoyaamini na
ninayoyaamini. Imani ni Matendo Na Matendo ni imani. Piga vita ufisadi kwa
imani na Matendo.
Moses Joseph Machali
X-mbunge, Kasulu Mjini 2010-2015,
0 Comments