Spika wa Bunge Mstaafu, Samuel Sitta (74) amefariki dunia usiku
wa kuamkia leo wakati akipatiwa matibabu nchini Ujerumani.
Mtoto wa marehemu, Benjamin Sitta amesema baba yake amefariki
saa 10:00 usiku wa kuamkia leo.
‘’Nikweli mzee amefariki nchini
Ujerumani akiwa anapatiwa matibabu, alipelekwa Alhamisi iliyopita na alikuwa
anasumbulia na saratani ya tezi dume ambayo ilisambaa na kuathiri miguu na
mwili mzima."
Benjamin amesema kuwa taarifa za mipango ya kusafirisha mwili
zitatolewa baadaye.
Sitta alikuwa Spika wa Bunge tangu mwaka 2005 hadi mwaka 2010 na
pia mbunge wa Urambo Mashariki.
Pia, alikuwa Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba na aliwahi
kuwa waziri katika wizara mbalimbali kwa vipindi tofauti.
Alikuwa miongoni mwa wanachama zaidi ya 42 wa CCM waliochukua
fomu za kugombea urais mwaka jana.
0 Comments