Mjini Kinshasa leo
(18.10.2016)vyama vinavyoshiriki katika serikali vimetia saini makubaliano
yanayotoa ruhusa kuchelewesha uchaguzi uliotarajiwa kufanyika katika Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Congo mwezi ujao.
Vyama vinavyounda muungano tawala katika
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na vyama vingine vidogo vimekubaliana
kuchelewesha uchaguzi wa mwezi ujao hadi Aprili mwaka 2018.
Vyama hivyo vimetia saini
makubaliano hayo mjini Kinshasa leo(18.10.2016). Makubaliano hayo yanatoa
nafasi kwa Rais Joseph Kabila kusalia madarakani hadi uchaguzi mpya
utakapofanyika.
Mkataba huo ulipitishwa
baada ya mazungumzo yaliyodumu kwa takriban siku 40,
chini ya usimamizi wa mjumbe wa Umoja wa Afrika Edem Kodjo, licha ya kususiwa
na vyama muhimu vya upinzani, kikiwemo UDPS cha kinara wa upinzani Etienne
Tshisekedi. Makubaliano hayo hayafafanui iwapo rais Kabila
anaweza kuwania muhula mwingine baada ya
mwaka huo.
Mahakama ya katiba katika nchi
hiyo vile vile imekubali ombi lililowasilishwa na tume
ya taifa ya uchaguzi la kuahirishwa uchaguzi wa rais na bunge
uliotarajiwa kufanyika mwaka huu. Hata hivyo mahakama
hiyo imeitaka tume hiyo ya uchaguzi kutangaza kalenda mpya ya
uchaguzi.
Vyama ambavyo
havikushiriki katika majadiliano hayo vinadai
kwamba Rais Kabila kubaki madarakani kupindukia
muda wake anaoruhusiwa na katiba ni kukiuka
katiba ya nchi hiyo.
0 Comments