Na Eric Amani – Dodoma
Watumishi wa Ofisi ya Rais –
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wametakiwa kuwa karibu zaidi na
watoto wao kwa kufuatilia kwa ukaribu mwenendo na malezi yao ili kujenga jamii
yenye maadili bora.
Wito huo umetolewa leo, Jumatatu Julai
21, 2025 na Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Dodoma, Mrakibu Msaidizi
wa Polisi (ASP) Christer Kayombo, wakati wa muendelezo wa mafunzo ya kila wiki
kwa watumishi wa ofisi hiyo.
ASP Kayombo amesema visa vingi vya
ukatili dhidi ya watoto vimekuwa vikichochewa na wazazi au walezi kushindwa
kuwajibika ipasavyo katika malezi ya watoto wao.
“Wazazi wengi wamekuwa wakiwatelekeza
watoto wao mikononi mwa wafanyakazi wa majumbani na hivyo kutoa mianya ya
vitendo vya ukatili na uhalifu kufanyika,” alisema ASP Kayombo na kuongeza:
“Tengeni muda wa kuwafuatilia watoto
wenu pindi mnapotoka kazini. Msiachie jukumu hilo kwa wengine. Simameni kama
walezi wa kweli na wenye kuwajali watoto.”
Aidha, aliwataka watumishi hao kuwa
mfano wa kuigwa katika jamii kwa kulea watoto wao katika misingi ya maadili
mema na kuimarisha mahusiano ya kifamilia.
Katika hatua nyingine, ASP Kayombo
aliwahimiza kuwa mabalozi wa kupinga vitendo vya ukatili—majumbani, maofisini
na katika jamii kwa ujumla.
“Ni matumaini yangu kuwa baada ya mafunzo
haya, matendo ya ukatili dhidi ya watoto na vitendo visivyofaa vitapungua
katika jamii,” alihitimisha ASP Kayombo.
0 Comments