WAKAZI WA SINGIDA WAILALAMIKIA SUWASA KWA UKOSEFU WA MAJI – MAMLAKA YATOA UFAFANUZI

 


 

Khadija Abdala wa Mtaa wa Mji wa zamani wa kwanza juu na Johari Juma wa Mtaa wa Nghongoajibu wa pili wakazi wa manispaa ya Singida wakilalamika kukosa maji.

Meneja wa Suwasa Singida Sebastian Warioba ametoa ufafanuzi kupita Meneja uzalishaji maji na usambazaji Mamlaka ya Maji Singida. 


SINGIDA

Baadhi ya wakazi wa Kata ya Mughanga na Mitaa ya Ghongwajibu, iliyopo katika Kata ya Kindai, Manispaa ya Singida, wameiomba Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Singida (SUWASA) kufafanua sababu za kutokuwepo kwa huduma ya maji kwa muda mrefu katika maeneo yao, hali ambayo imesababisha usumbufu mkubwa kwa jamii bila taarifa yoyote rasmi kutoka kwa mamlaka hiyo.

Wakizungumza katika semina ya siku moja iliyoandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji Kanda ya Kati (EWURA), wakazi hao walieleza kuwa wamekuwa wakikosa huduma hiyo ya msingi kwa kipindi kirefu na kuona kimya cha mamlaka hiyo kama kutowajali walaji.

“Hali ni ngumu, maji hayapatikani kabisa na hakuna hata taarifa. Hatujui tuamini nini,” alisikika mkazi mmoja akilalamika mbele ya wawakilishi wa EWURA.

SUWASA Yatolea Ufafanuzi

Kufuatia malalamiko hayo, blogu hii ilifika katika ofisi za SUWASA mjini Singida kufuatilia suala hilo. Meneja wa Uzalishaji Maji na Usambazaji kutoka SUWASA, Mhandisi Elisha Kivuyo, alitoa ufafanuzi kuhusu chanzo cha changamoto hiyo.

Kulingana na Mhandisi Kivuyo, tatizo hilo lilisababishwa na kuharibika kwa mota ya kusukuma maji katika kisima cha LITI kilichopo Kata ya Ipembe, jambo lililoathiri upatikanaji wa huduma ya maji katika baadhi ya maeneo ya Kata za Ipembe na Kindai, ikiwa ni pamoja na vitongoji kadhaa vilivyopo pembezoni.

“Hili ni tatizo la kiufundi lililotokea ghafla. Mota ya kusukuma maji iliharibika, jambo lililosababisha usumbufu mkubwa. Hata hivyo, tunapenda kuwataarifu wananchi kuwa mota hiyo tayari imetengenezwa na huduma ya maji imeanza kurejea kwa awamu,” alisema Mhandisi Kivuyo.

Aliongeza kuwa licha ya changamoto hiyo ya kifundi, SUWASA inaendelea kuchukua hatua za kudumu za kuboresha miundombinu ya maji ili kuhakikisha huduma inapatikana kwa uhakika na kwa wakati kwa wakazi wa Manispaa ya Singida.

“Tunaelewa umuhimu wa maji kwa wananchi, na ndio maana tunafanya kazi usiku na mchana kurejesha huduma hiyo. Tunaomba radhi kwa usumbufu uliojitokeza,” aliongeza Kivuyo.

Tuandikie Maoni Yako Hapa

Post a Comment

0 Comments