Wataalamu mbalimbali kutoka EWURA kanda ya kati na Jeshi la Zimamoto mkoa wa Singida wakitoa Elimu juu ya kujikinga na majanga ya Moto.

SINGIDA DIGITAL
Wakazi wa Mkoa wa Singida waliokusanyika kwa ajili ya semina ya siku moja kuhusu matumizi salama ya gesi ya kupikia wameipongeza Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), kwa hatua yake ya kuwakutanisha wadau na kutoa elimu muhimu kuhusu usalama wa matumizi ya nishati hiyo.
Semina hiyo ilifanyika katika ukumbi wa RC Mission mjini Singida na
kuhudhuriwa na wauzaji na watumiaji wa gesi kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa
huo. Lengo kuu la semina ilikuwa ni kutoa mwanga juu ya matumizi bora ya gesi,
namna ya kuhifadhi mitungi kwa usalama, na hatua za tahadhari ili kuepuka ajali
zinazotokana na uzembe au uelewa mdogo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya washiriki waliishukuru
EWURA kwa kuandaa semina hiyo na kuomba elimu hiyo isambae hadi vijijini ambako
bado kuna uelewa mdogo wa matumizi salama ya gesi ya kupikia.
“Tumejifunza mambo muhimu sana kuhusu usalama wa mitungi yetu na
matumizi ya gesi majumbani. Tunaiomba EWURA iende mbali zaidi, hasa vijijini
ambako watu bado wana wasiwasi kutumia gesi,” alisema mmoja wa washiriki.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa EWURA kanda ya kati, Bi Hawa Luweno,
alisema kuwa semina hiyo ni sehemu ya jitihada za mamlaka hiyo kuhakikisha
wananchi wanatumia nishati safi kwa usalama, huku wakielewa haki na wajibu wao
kama watumiaji.
“Tulikuja kusikiliza maoni yao, kuzijua changamoto, na kuwapa elimu
inayotakiwa ili waendelee kutumia gesi kwa usalama,” alisema Bi Luweno.
EWURA imeahidi kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu matumizi
salama ya nishati, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kuhamasisha
matumizi ya nishati safi kwa ajili ya afya ya jamii na uhifadhi wa mazingira.
0 Comments