MASHAURI TISA YA JINAI KUSHUGHULIKIWA SINGIDA


Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo (kushoto) akielezea jambo katika kikao cha kusikiliza mashauri ya jinai mkoani Singida. Aliyeketi kushoto kwa Jaji Mfawidhi ni Naibu Msajili Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe. Sylivia Lushasi.

Naibu Msajili Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Mhe.Sylivia Lushasi akifafanua jambo katika kikao cha kusikiliza mashauri ya jinai mkoani Singida.


Kaimu Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Singida (aliyesimama) Mhe. Fadhili Luvunga  akitoa neno la shukrani katika kikao cha kusikiliza mashauri ya jinai mkoani Singida.

Mwakilishi kutoka Gereza la Wilaya Singida, Bw.Lakwanti akitoa taarifa fupi katika kikao hicho.
Sehemu ya wajumbe kutoka Ofisi ya Upelelezi Mkoani Singida, Ofisi ya Mashataka Mkoa na Mawakili wa Kujitegemea waliohudhuria kikao hicho.

Na  Mahakama, Singida


Jumla ya mashauri tisa (9) yanatarajiwa kumalizwa katika kikao cha mwezi mmoja cha kusikiliza mashauri ya jinai mkoani Singida ikiwa ni kikao cha kwanza kwa mwaka 2024.


Katika taarifa ya ufunguzi iliyosomwa leo tarehe 06 Mei, 2024 na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma Mhe, Sylivia Lushasi ameeleza kuwa, jumla ya mashauri tisa (9) ya jinai yanatarajiwa kushughulikiwa ndani ya mwezi mmoja kuanzia tarehe leo hadi tarehe 04 Juni, 2024 na kuongeza kwamba, Mashauri 06 yanatoka Singida, shauri moja (01) Manyoni na Iramba mashauri mawili (02).


“Sambamba na taarifa hii, Mkoa wa Singida una mashauri 31 ambayo yanasubiri kusikilizwa (uncauselisted) ambapo Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida kuna mashauri 16, Iramba 08 na Manyoni 07,” amesema Mhe. Lushasi.


Mhe. Lushasi amebainisha kuwa mashauri tajwa hayahusishi mashauri yanayosubiri washtakiwa kusomewa kwa mara ya kwanza (plea taking).
Aidha, amewashukuru Wadau kwa ushirikiano wanaouonesha na kuomba umoja na mshikamano uendelee kwani vikao hivi vimekuwa vikifanikiwa kwa kiasi kikubwa na kufikia malengo.


Naye, Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt Juliana Masabo amewapongeza Wadau kwa ushirikiano ambao wamekuwa wakiuonesha katika kufanikisha usikilizwaji wa mashauri na kuendelea  kusisitiza Mawakili na Wadau kunyumbulika (flexibility), kusoma majalada vizuri na kuongea na wateja wao vizuri.


Vilevile amewasisitiza Magereza kuhakikisha Mahabusu ambao wako mbali kuwa wanafikishwa mapema angalau wiki moja kabla ya kikao kuanza ili waweze kupata muda wa kuzungumza na Mawakili wao.


Hata hivyo, Wadau kwa pamoja wamehaidi kuendelea kutoa ushirikiano mkubwa na wamejipanga vizuri hasa Ofisi ya Mashtaka wameomba vikao vifanyike mara kwa mara kwani kwa sasa wana bajeti ya kutosha kuwezesha mashahidi.


Tuandikie Maoni Yako Hapa

Post a Comment

0 Comments