Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe.
Nape Moses Nnauye (Mb), amethibitisha kuwa mradi wa kupeleka mawasiliano ya
simu vijijini ambao ni ujenzi wa minara 758, utakamilika ifikapo mwaka 2025.
Waziri Nape alitoa kauli hiyo alipokuwa akitoa
maelezo mbele ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu wakati wa
ziara katika eneo la ujenzi wa mnara wa mawasiliano ya simu katika Kijiji cha
Itaga, Kata ya Misha, Tabora.
Waziri Nape alisema kuwa mikataba inayohusiana na
mradi huo inatakiwa ikamilike ifikapo Februari 2025, na kuongeza kuwa kabla ya
uchaguzi mkuu, minara yote itakuwa imewashwa na watu zaidi ya milioni 8
watakuwa wameunganishwa na mtandao.
Aliongeza kuwa, Serikali imepanga kuzindua zaidi
ya minara 100 ambayo tayari imekamilika kwa awamu ya kwanza wakati wa sherehe
za miaka 60 ya Muungano mwaka huo.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Selemani Moshi
Kakoso (Mb), aliitaka Serikali kuhakikisha kuwa Wizara itamaliza ujenzi wa
minara hiyo kwa wakati, akisisitiza kuwa mawasiliano ni muhimu kwa jamii katika
kuwezesha uchumi wa kidijitali.
Mhe. Kakoso pia alipongeza Wizara kwa jitihada
zake za kuboresha huduma za mawasiliano nchini, pamoja na mafanikio
yaliyopatikana katika zoezi la operesheni Anwani za Makazi.
Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote
(UCSAF), Bi. Justina Mashiba, alisema kuwa Serikali kupitia mfuko huo imetoa
ruzuku ya shilingi milioni 320 kwa Shirika la Mawasiliano Tanzania TTCL kwa
ajili ya ujenzi wa minara 34 ya mawasiliano katika maeneo maalum nchini.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Shirika la
Mawasiliano Tanzania (TTCL), Mhandisi Peter Ulanga, alisema kuwa minara mingi
inayojengwa na shirika hilo inaunganishwa na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, na
hivyo kasi ya mawasiliano imekuwa kubwa.
Minara hiyo 758 inajengwa kwa ushirikiano kati ya
Serikali kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na
kampuni mbalimbali za mawasiliano nchini, ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alizindua mradi huo tarehe 13 Mei 2023
katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete, Dodoma.
0 Comments