Eneo la machimbo ya Almasi lililo chimbwa tangu enzi hizo katika muonekano wa sasa. |
Na Mwandishi wetu Shinyanga.
Serikali
kwa kushirikiana na Kampuni Williamson Diamond inaweka mikakati mbalimbali ya
kukabiliana na changamoto ya kushuka kwa bei ya madini ya almasi katika soko la
Dunia kutokana na kuibuka kwa almas inayotengenezwa katika Maabara na
kuongezeka kwa mahitaji ya madini mengine.
Hayo yalielezwa na Waziri wa Madini Mhe.Anthony
Mavunde wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya Mgodi wa uchimbaji na
uzalishaji wa madini ya almasi katika mgodi wa Mwadui wa Williamson Diamond Ltd
(WDL) mkoani Shinyanga.
Waziri Mavunde alisema kuwa, kwasasa duniani kuna
uhitaji wa madini mengine ambayo nayo yanahitajika katika sehemu mbalimbali
duniani hivyo kupelekea madini kuwa katika ushindani.
Waziri Mavunde alifafanua kuwa, Tanzania ni
mwanachama wa umoja wa nchi zinazozalisha almasi Afrika(ADPA), hivyo kupitia
umoja huo nchi wazalishaji zimeendelea kujadili mikakati ili kurudisha thamani
ya almasi katika masoko ya ununuzi na hasa katika kukabiliana na almasi ya
maabara.
Kwa upande wake, Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya
Bunge ya Kudumu ya Nishati na Madini Mhe.Masache Kasaka aliupongeza mgodi kwa
kazi nzuri inayofanywa na Menejimenti ya Uongozi wa mgodi hususani katika
jitihada walizofanya za kukabiliana na athari kwa jamii pindi bwawa la
kuhifadhi maji lilipopasuka na kuitaka Menejimenti ya Mgodi kusimamia na
kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na Kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati
na Madini ilipotembelea hapo.
Naye,Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mh. Anamringi Macha
aliutaka mgodi kuendelea kujenga mahusiano mazuri na wachimbaji wadogo
wanaochimba almasi pembeni ya mgodi kwa kuwashirikisha na kuwasaidia namna bora
ya kufanya uchimbaji bila kuathiri maeneo yanayozunguka mgodi hii itakuwa faida
kwa mgodi na mkoa kwa ujumla.
Awali , akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya
mgodi, Mkurugenzi Mtendaji wa Mgodi , Ndg.Ayubu Mwenda alisema mgodi unaendelea
na uzalishaji changamoto kubwa ni kushuka kwa bei kutokana na kuibuka kwa
almasi inayotengenezwa katika maabara ambayo inauzwa kwa bei ya chini na kuleta
ushindani katika soko.
Mwenda aliongeza kuwa, mgodi unauwezo wa kuendelea
kuzalisha almasi kwa kipindi cha miaka hamsini ijayo hii ni kutokana na
makadirio ya mashapo yaliyopo mgodini.
0 Comments