Na Ras Singida
Wadau mbalimbali wa sekta binafsi wameweza kuongeza nguvu katika
kuboresha sekta ya Afya Mkoani Singida kutokana na ushirikiano mzuri ulipo
baina yao na serikali.
Hayo yamebainishwa katika mkutano maalumu wa siku mbili
uliohitimishwa jana Mjini Singida, ambapo viongozi wa serikali, taasisi na
mashirika 15 yanayotoa huduma za Afya na Ustawi wa jamii Mkoani hapa
wamejadiliana namna ya kuboresha ushirikiano baina yao.
Mratibu wa Ukimwi Mkoa wa Singida Dkt Mohamed Mbalazi amesema
katika mapambano dhidi ya Ukimwi na Virusi vya Ukimwi (VVU) Mkoani hapa, Sekta
binafsi zimekuwa na mchango mkubwa.
Dkt Mbalazi amesema wadau hao wameweza kutoa dawa za kupunguza
makali ya VVU, tiba lishe, mafunzo kwa watoa huduma wa afya, ufuatiliaji wa
watumia wa dawa za VVU pamoja na kuandaa takwimu jambo ambalo limeboresha
mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi.
“Sisi kama watendaji wa serikali tunathamini na kutambua mchango
wa wadau wa sekta afya kwakuwa ni nguzo muhimu sana, mfano wadau wetu shirika
la EGPAF, wametenga bilioni 1.6 kwa ajili ya mapambano dhidi ya Ukimwi na
maambukizi ya VVU” Mkoani Singida”, amesema na kuongeza kuwa,
“Fedha hizo zitaongea nguvu pale ambapo kuna changamoto au
bajeti inakuwa haitoshelezi, lakini pia tunaendelea kutoa wito kwa wadua
wengine waendelee kuongea nguvu na wigo wa ushirikiano kwakuwa lengo letu ni
moja yaani kumsaidia mwananchi apate huduma bora za afya”, amesisitiza Dkt
Mbalazi.
Naye Afisa Lishe Mkoa wa Singida Teda Sinde amesema wadau
wamekuwa watekelezaji wazuri wa masuala ya Lishe Mkoani hapa hasa kwa ngazi ya
jamii hivyo ushirikiano kati yao umekuwa wa manufaa makubwa.
Teda amesema mkutano huo wa wadau umewawezesha watendaji na
viongozi wa serikali kuelewa kwa upana zaidi kazi wanazofanya wadau pamoja na
changamoto wanazopitia ili waweze kusaidiana katika kuboresha hali ya Lishe
Mkoani hapa.
“Mkutano huu umeongeza na kuboresha ushirikiano baina yetu na
wadau wetu ambao wengi wao wanatoa chakula lishe na elimu ya lishe kwa akina
mama wajawazito, watoto wenye umri wa miezi sita mpaka 59 na akina mama
wanaonyonyesha watoto chini ya miezi sita”, ameeleza Teda.
Ameongeza kuwa mkutano huo umeweza kusaidia katika kupanga
mikakati ya utoaji huduma ili kuepusha wadau wanaotoa huduma ya aina moja
kutoelekeza nguvu katika maeneo yanayofanana au ambayo hayana uhitaji mkubwa
kuliko mengine.
Akifungua Mkutano huo Mwakilishi wa Kaimu Katibu Tawala Mkoa,
Cosmas Sikali aliwataka wadau kujadili sera, sheria, kanuni, maeneo ya
kipaumbele katika miradi mbalimbali, mafanikio na changamoto katika utekelezaji
wa mipango mikakati inayosisitiza ushirikiano kati ya Sekta ya Umma na binafsi.
Sikali amesema endapo nguvu hizi kwa pamoja zitaunganishwa na
kuratibiwa vizuri kwa kiasi kikubwa changamoto zilizopo katika sekta ya afya na
ustawi wa jamii pamoja na maradhi kwa wananchi yataweza kupungua.
Ameongeza kuwa serikali peke yake haitaweza kufikia malengo ya
kupunguza vifo vya watoto, akina mama wajawazito na kuweza kudhibiti magonjwa
ya kuambukiza na yasiyoambukiza, pamoja na kuboresha afya ya
mazingira na kupata maji safi na salama bila kushirikiana na Sekta
binafsi.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Salum
Manyatta amesema mkutano huo umeshirikisha wadau wote muhimu wanatoa huduma za
afya na ustawi wa jamii mkoa wa Singida.
Dkt Manyatta amesema mkutano huo umeweka malengo na maazimio ya
pamoja na wadau wa sekta binafsi ili kuimarisha sekta ya afya na ustawi wa
jamii Mkoani Singida.
Mratibu wa Ukimwi Mkoa wa Singida Dkt Mohamed Mbalazi akitoa
mada katika mkutano ulijadili uboreshaji wa ushirikiano baina ya serikali na
wadau wa sekta binafsi zinazotoa huduma ya Afya Mkoani Singida.
Afisa Lishe Mkoa wa Singia Teda Sinde akifafanua jambo katika
mkutano ulijadili uboreshaji wa ushirikiano baina ya serikali na wadau wa sekta
binafsi zinazotoa huduma ya Afya Mkoani Singida.
Mratibu wa Kifua Kikuu na Ukoma Mkoa wa Singida Dkt Evans
Mlay (wa kwanza kushoto) akipitia dondoo, kabla ya kuwasilisha mada
iliyoonyesha mchango mkubwa wa wadau Sekta ya Afya katika mapambano dhidi ya
Kifua Kikuu Singida, Kulia kwake ni Afisa Mradi wa AMREF Mkoa wa Singida
Donathapeace Kayoza.
Mwakilishi wa Kaimu Katibu Tawala Mkoa, Cosmas Sikali
akizungumza na wadau wa sekta binafsi zinazotoa huduma katika Mkoa wa Singida.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Salum Manyatta akisikiliza
kwa makini maoni na michango mbalimbali ya wadau ambao ni taasisi na mashirika
binafsi yanayotoa huduma za Afya Mkoani Singida.
Meneja Mradi wa EGPAF Kanda ya Kati Dkt Joseph Obedi akiandika
baadhi ya mapendekezo ya kuboresha ushirikiano kati ya sekta binafsi na
serikali katika uboreshaji wa huduma za Afya Mkoa wa Singida.
0 Comments