Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli
amelifuta agizo lililotolewa waziri wa katiba na Sheria Dkt. Harrison Mwakyembe
linalowataka watu wote wanaotaka kufunga ndoa kuwa na cheti cha kuzaliwa
kuanzia tarehe mosi mwezi Mei 2017.
Magufuli amefuta agizo wakati akizungumza na waandishi wa habari
muda mfupi kabla ya kuondoka katika Ikulu ya Chamwino Mkoani Dodoma na kurejea
Jijini Dar es Salaam.
Kiongozi huyo amesema kuwa serikali haiwezi kuruhusu sharti hilo
kutumika kwa kuwa litawanyima haki ya kuoa na kuolewa Watanzania wengi ambao
hawana vyeti vya kuzaliwa, huku utaratibu wa kupata vyeti hivyo ukiwa bado
unakabiliwa na changamoto nyingi kwa wanaohitaji.
Amesema hadi kufikia sasa idadi ya Watanzania walio na vyeti vya
kuzaliwa ipo chini ya asilimia 20 huku wengi wao wakiwa ni wananchi wanaoishi
vijijini ambako ni vigumu kupata vyeti hivyo, na wengine wakiwa ni waliozaliwa
kabla ya kuanza kutolewa kwa vyeti vya kuzaliwa nchini mwaka 1961.
''Kwa hiyo ndugu zangu Watanzania msiwe na wasiwasi wowote,
endeleeni na utaratibu wenu wa kuoa na kuolewa kama kawaida na kama kuna
kifungu chochote cha sheria kinachomlazimisha mtu awe na cheti cha kuzaliwa
ndipo aoe ama aolewe nitamuelekeza waziri wa katiba na sheria Mhe. Harrison
Mwakyembe apeleke bungeni kikarekebishwe" amesema Magufuli.
Wakati huohuo Magufuli ametoa wito kwa wanasheria kuzikagua
vyema sheria zinazohusiana na kuzaliwa na kifo na kuoa na kuolewa ili zisilete
mkanganyiko kwa wananchi.
Hata hivyo rais Magufuli ametoa wito kwa Watanzania kuendelea
kupata vyeti vyao vya kuzaliwa kama kawaida na amewataka viongozi wote
kuwahamasisha wananchi kuwa na vyeti hivyo.
0 Comments