Mh Mwigulu Nchemba Waziri wa mambo ya Ndani |
WAZIRI wa mambo ya ndani Mwigullu Lameck
Nchemba,ameliagiza jeshi la polisi nchini,kuwakamata na kuwafikisha kwenye
vyombo vya sheria madereva wanaoacha mawe na matawi ya miti
barabarani.
Nchemba ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Iramba
mkoani hapa,ametoa agizo hilo juzi wakati akizungumza kwenye kikao cha 38 cha
bodi ya barabara mkoa kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu
wa mkoa mjini hapa.
Alisema baadhi ya madereva wa magari na hasa
yale makubwa,hutumia mawe kuzuia magari yao kutembea wakati wakiyafanyia
matengenezo ya dharura.
“Wakiisha maliza kuyafanyia matengenezo magari
yao,madereva hao huyaacha barabarani mawe na matawi ya miti ambayo hutumika
kutoa tahadhari kwa vyombo vingine vya moto.Kitendo hicho kinahatarisha maisha
na mali za watumiaji wengine wa barabara, kwa vile yanaweza
kusababisha ajali”,alisema Mwigullu.
Kwa hali hiyo,alisema jeshi la polisi linapaswa
kuimarisha mawasiliano ili waweze kuwathibiti na kuwakamata madereva wanaoacha
mawe na matawi ya miti barabarani.
Katika hatua nyingine,waziri huyo alisema upo
umuhimu mkubwa wananchi na hasa wale wanaoishi kando kando ya
barabara,kuelimishwa juu ya matumizi bora ya barabara zinazojengwa kwa fedha
nyingi,ili waweze kuacha kupitisha mifugo yao na mikokoteni barabarani.
Kwa upande wake mwenyekiti wa bodi ya barabara
na mkuu wa mkoa wa Singida,mhandisi Mathew John Mtigumwe,aliagiza kuwa fedha
zinazotolewa na serikali na wafadhili mbalimbali wa miradi ya barabara,matumizi
yake yasimamiwe kikamilifu, ili zitumike kwa miradi iliyokusudiwa.
“Ujenzi wa miradi hiyo ya barabara ufanane na
thamani halisi ya fedha zilizotumika.Pia kazi za ujenzi wa barabara za ngazi
zote,wapewe wakandarasi bora na wenye uwezo wa kutekeleza miradi ikakamilika
kwa wakati.Nasisitiza kuimarishwa kwa usimamizi na ukaguzi wa mara kwa mara wa
miradi ya barabara ili barabara ziwe za kiwango kinachokusudiwa”,alisema.
Wakati huo huo,mhandisi Mtigumwe ambaye kabla ya
kuteuliwa kuwa mkuu wa mkoa alikuwa meneja TANROADS mkoa,alitumia fursa hiyo kuupongeza
uongozi wa TANROADS mkoa wa Singida chini ya meneja wale Eng.Leonard
Kapongo,kwa kazi nzuri ya usimamizi na ukaguzi,uliopelekea miradi ya barabara
kujengwa kwa ubora unaofafana na fedha zilizotumika.
0 Comments