AZAM FC imecheza mechi ya sita mfululizo ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania
Bara bila ushindi, kufuatia kulazimishwa sare ya 1-1 na Mtibwa Sugar usiku huu
Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Mara ya mwisho, Azam ilishinda mechi ya Ligi Kuu Septemba 10, mwaka huu
ilipoilaza 2-1 Mbeya Uwanja wa Sokoine.
Kutoka hapo, ikafungwa 1-0
na Simba Septemba 17, 2-1 na Ndanda FC mjini Mtwara Septemba 24, sare ya 2-2 na
Ruvu Shooting Chamazi Oktoba 2, kabla ya kufungwa 1-0 na Stand United mjini
Shinyanga Oktoba 12 na sare ya 0-0 na Yanga Oktoba 16 Dar es Salaam.
Katika mchezo wa leo, Mtibwa Sugar walianza kupata bao lililofungwa na
mshambuliaji wake, Rashid Mandawa dakika ya pili, kabla ya kiungo Himid Mao
kuisawazishia Azam kwa penalti dakika ya 11.
Penalti hiyo ilitolewa baada ya mchezaji mmoja wa Mtibwa Sugar kuunawa
mpira kwenye boksi na kwa matokeo hayo, Azam FC inajiongezea pointi moja na
kufikisha 13 baada ya kucheza mechi 10.
Mtibwa Sugar inafikisha pointi 16 baada ya kucheza mechi 11. Mechi
nyingine za leo, Yanga SC imeshinda 2-0 dhidi ya Toto Africans mjini Mwanza,
Ruvu Shooting imetoa sare ya 1-1 na Mwadui, Ndanda
1-1 na Mbeya City mjini
Mtwara, Prisons imeshinda mabao 2-1 dhidi ya Stand United na African Lyon
imefungwa 2-0 na Maji Maji, wakati kesho Simba watakuwa wenyeji wa Mbao FC.
0 Comments