Grace Gwamagobe-Songwe.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Chiku Gallawa amesema atahakikisha
anasimamia kwa ukaribu fedha zilizotolewa na serikali Mkoani hapa kwa ajili ya
upanuzi wa vituo vya afya ili zifanye kazi zaidi ya ile iliyopangwa awali
kutokana na kuongezeka kwa nguvu za wananchi.
Gallawa ameyasema hayo mapema jana wakati wa ziara yake Wilaya
ya Mbozi alipokagua maendeleo ya upanuzi wa vituo vya afya vya Isansa
kilichopokea milioni 500 na kituo cha Afya cha Iyula Kilichopokea milioni 400,
kwa ajili ya ujenzi wa maabara, nyumba ya daktari, chumba cha upasuaji, jengo
la mama na mtoto na chumba cha kuhifadhia maiti.
“Fedha hizi lazima zifanye kazi iliyopangwa vizuri na pia
tuongeze kazi nyingine ya ziada kutokana na kuwa tumepata nguvu ya wananchi
lakini pia mafundi wetu hawa tunaowatumia ni wazawa na wenyeji wa maeneo ya
kwetu kwahiyo gharama zao zitatupa unafuu ambao tunatakiwa kuutumia kuongeza
kazi nyingine”, amesema Gallawa.
Ameongeza kuwa licha ya upanuzi wa vituo vya afya kuchelewa
kuanza bado ana Imani kuwa wataweza kumaliza ndani ya muda uliopangwa kutokana
na uchapakazi wa mafundi wazawa wa maeneo hayo.
Gallawa ames
ema kukamilika upanuzi wa vituo hivyo vya afya kutavifanya vituo
hivyo vivutie na hata mgonjwa akifika apate matumaini ya kupona na sio
kukatishwa tamaa na hali mbovu ya mazingira.
“Tiba ya kwanza ya mgonjwa akifika kituo cha afya akute
mazingira yanavutia na sio majengo mabovu na uchafu hivyo vitamfanya akate
tamaa ya kupata matibabu sahihi, tukimaliza ujenzi wa hayo majengo
tutahakikisha tunapaka rangi paa za majengo yote zifanane ili vituo vyetu vya
afya vivutie”, amefafanua Gallawa.
Aidha Gallawa amemtaka Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya
ya Mbozi Lauteri Kanoni kuhakikisha anaweka mfumo wa maji safi katika vituo
hivyo hasa mfumo wa kuvuna maji ya mvua ili vituo vikikamilika maji yawepo kwa
ajili ya matumizi.
Naye Mkazi wa kijiji cha Isansa Wilaya ya Mbozi Bi Stela Mkeya
ameonyeshwa kufurahishwa na upanuzi wa kituo cha Afya Isansa huku akieleza
baadhi ya kero walizokuwa wakizipata awali.
“Tunaishukuru sana serikali ya Magufuli kwakweli wametusaidia,
tulikuwa tunapata shida kufuata huduma za upasuaji wa akina mama wajawazito
huko hospitali ya Wilaya iliyopo Vwawa lakini pia hapa kwenye kituo cha afya
mzazi akijifungua hata mazingira ya kwenda kujisafisha vizuri kama vile mabafu
yakiwa hayatoshi kabisa”, ameeleza Bi Mkeya.
Kwa upande wao mafundi waliokabidhiwa kazi ya upanuzi wa vituo
hivyo vya Afya wameonyesha ari ya kufanya kazi hiyo kwa ufanisi na haraka huku
wakimuomba Mkuu wa Mkoa Chiku Gallawa awasaidie upatikanaji wa taa ili waweze
kufanya kazi mchana na usiku naye Mkuu wa Mkoa amekubaliana na mapendekezo
hayo.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Chiku Gallawa akizungumza na mafundi
wanaojenga katika kituo cha Afya Isansa Wilaya ya Mbozi, kituo hicho cha Afya
kimepokea shilingi milioni 500 kwa ajili ya upanuzi wa kituo hicho.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Chiku Gallawa akizungumza na baadhi ya
watendaji na wananchi wa kijiji cha Iyula waliojitokeza katika eneo la ujenzi
katika kituo cha Afya cha Iyula Wilaya ya Mbozi, kituo hicho cha Afya kimepokea
shilingi milioni 400 kwa ajili ya upanuzi wa kituo hicho.
0 Comments