JUMLA YA MAGOGO 297 YAMETAIFISHWA NA SERIKALI WILAYANI MANYONI



Na,Jumbe Ismailly ITIGI     
SHEHENA nyingine ya magogo 297 yenye thamani ya shilingi milioni 26,370,000/= yaliyokuwa yakimilikiwa na Kampuni ya ARIZONA ENTERPRISES iliyopo katika Mji mdogo wa Itigi, wilayani Manyoni,Mkoani Singida yametaifishwa na serikali wilayani Manyoni na hivyo kufanya jumla ya magogo 720 yaliyotaifishwa na serikali baada ya kubainika kwamba mmiliki wa kampuni hiyo alikiuka taratibu za uvunaji wa mazao ya misitu.
Mapema mwezi Oktoba,2017 serikali wilayani Manyoni ilitaifisha shehena ya magogo 423  yenye thamani ya shilingi milioni 283,022,000/= yaliyokuwa yamefichwa kwenye mashamba ya Mbunge wa Jimbo la Manyoni Magharibi,Bwana Yahaya Masare katika Kijiji cha Damwelu,kata ya Ipande,wilayani Manyoni,baada ya mmiliki wa mashamba hayo  kuyakana kuwa siyo mali yake,licha ya kwamba mmoja wa watu waliokuwa wakishikiliwa na polisi wilayani Manyoni,Bwana Hassani Masare ni ndugu yake.
Akithibitisha shehena ya mazao  hayo ya misitu kutaifishwa,Afisa Ardhi na Maliasili Halmashauri ya Itigi,Bwana Rodney Ngalamba amesema baada ya kukamilisha taratibu za kisheria,mtuhumiwa au mshukiwa wa magogo hayo ameweza kulipa serikalini faini ya shilingi milioni 46.
Kwa mujibu wa afisa huyo mwenye dhamana ya kusimamia maendeleo ya ardhi na Maliasili ameweka bayana pia kwamba katika upekuzi iligundulika kwamba kulikuwa na ukiukwaji wa sheria kwa maana baadhi ya shehena katika kiwanda ARIZONA ENTERPRISES kilichopo mjini Itigi kulikuwa na mzigo zidifu wa magogo 297.
Akizungumzia kuhusu hatua itakayofuata baada ya mtuhumiwa kutozwa adhabau ya faini,Bwana Ngalamba ameweka bayana kuwa shehena hiyo ambayo imetaifishwa na serikali itauzwa kwa njia ya mnada na baada ya kupatikana kwa nyaraka zinazohalalisha mzigo uliopo kiwandani,mmiliki wa Arzona Enterprises ataweza kurudishiwa ili aweze kuendelea na shughuli zake za uchakataji wa magogo hayo.
Kwa upande wake Mwanasheria wa Halmashauri hiyo,Bwana Gilbert Modesti Kalanda aliyekuwa mmoja wa wajumbe sita wa tume iliyokwenda Kaliua,amesema akiwa mmoja wa wajumbe wa Tume hiyo  walikwenda Mkoani Tabora,na wilayani Kaliua kwenye eneo ulikotoka mzigo huo la Mpandaline mpakani mwa Kaliua na Katavi.
Kwa mujibu wa Bwana Kalanda baadhi ya mapendekezo ya tume hiyo yalikuwa ni pamoja na kuainisha makosa ya kukutwa na mazao ya misitu bila kufuata sheria na walimtaka mtuhumiwa kulipa shilingi milioni 26,370,000/= ambazo ni gharama za mzigo wote.


Tuandikie Maoni Yako Hapa

Post a Comment

0 Comments