Kocha Mkuu wa Yanga SC, Mholanzi Hans van der
Pluijm amejiuzulu pamoja na benchi lake zima na amesema hataki kufanya kazi
kama Mkurugenzi wa Ufundi.
Amesema hatua hiyo inatokana na uongozi wa
klabu kuleta kocha mpya, Mzambia George Lwandamina bila kumtaarifu, akisema
huko ni kumvunjia heshima.
Pluijm amesema kwamba alipaswa kutaarifiwa na
uongozi juu ya jambo lolote kuhusu nafasi yake kazini, lakini ajabu anajua
kupitia vyombo vya habari.
Pluijm amekerwa na kitendo cha uongozi kuleta
kocha mpya yeye akiwa kazini. “Sijaambiwa chochote. Uongozi umenivunjia heshima
sana, kwa klabu kama Yanga SC hawakupaswa kufanya hivyo,”alisema Pluijm.
Aidha, kuhusu uwezekano wa kuwa Mkurugenzi wa
Ufundi, Pluijm alisema; “Sipendelei hiyo kazi. Nataka kufanya kazi na wachezaji
kila siku kwa matakwa ya moyo wangu. Ninaondoka, mimi ni kocha mkubwa na nina
wasifu mzuri. Nitapata timu,”alisema.
Pluijm anaondoka siku mbili kabla ya Yanga
kucheza na JKT Ruvu katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Jumatano.
Yanga imerejea leo kutoka Mwanza, ilikopita
ikitokea Bukoba, mkoani Kagera ambako Jumamosi ilishinda 6-2 dhidi ya wenyeji
Kagera Sugar katika mfululizo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Uongozi wa Yanga unamuondoa Pluijm na
Wasaidizi wake wote, Juma Mwambusi, kocha wa makipa Juma Pondamali na Meneja
Hafidh Saleh wote wazalendo na kumpa nafasi Mzambia, George Lwandamina
atakayekuwa Kocha Mkuu, akisaidiwa na wazalendo Charles Boniface Mkwasa,
Manyika Peter kocha wa makipa na Meneja, Sekilojo Chambua.
0 Comments