WAKULIMA WA ZAO LA ALIZETI MKOANI SINGIDA WAPATA UHAKIKA WA MBEGU



Wakulima wa zao la alizeti Mkoani Singida wamepata uhakika wa mbegu bora ya alizeti ambayo itawasaidia kuzalisha kibiashara tofauti na hapo awali walipokuwa wakipata mbegu zisiso na uhakika wa mavuno mazuri.

Mwenyekiti wa chama cha Wakulima wa Alizeti Mkoa wa Singida Athumani Sima amesema hayo mapema leo katika mkutano wa wadau wa kilimo cha alizeti ulioandaliwa na mradi wa Faida Mali kupitia Shirika la AMDT ambalo limejikita katika kusaidia wakulima wa zao hilo kupata mbegu bora.

Sima amesema hapo awali wakulima walikuwa wakinunua mbegu kwa wauzaji ambao sio waaminifu na hivyo kutovuna vizuri kutokana na mbegu hizo kuota vibaya na kutoa alizeti kidogo.

Amesema mradi wa Faida Mali umewahakikishia kuwasaidia upatikanaji wa mbegu bora na ya kisasa na hivyo kukifanya kilimo cha alizeti kuwa kama biashara nyingine ambazo zina faida kubwa.

“Hawa Faida Mali sisi tunawaamini kwakuwa wamekuwa wakishirikiana na serikali hivyo watatusaidia katika kupata mbegu bora, tulikuwa tunaumizwa na wauzaji wengine akikuuzia mbegu inaota hapa, pale haioti matokeo yake unapata hasara” amesema na kuongeza kuwa,

“Mkulima akipata Mbegu bora hiyo ni hatua ya kwanza ya mafanikio, kwakweli baadhi yetu tulianza kukata tamaa kwa kuona tunapata hasara tu, unalima alizeti miaka mingi huoni faida kubwa kama ambavyo unatarajia, lakini mradi huu umetuonyesha njia ya mafanikio, nawaomba wakulima wengine waweze kujiunga katika vikundi ili waweze kufikiwa na mradi huu au miradi mingine”, amesisitiza.

Naye Mkulima wa alizeti Kutoka kata ya Kinampundu Wilaya ya Mkalama Samwel Laida amesema utaratibu wa kununua alizeti kwa magunia ya lumbesa badala ya vipimo vya mizani unawapunja wakulima na kuwafanya warudi nyuma kiuchumi.

Laida amesema wanunuzi wa alizeti wanapakia alizeti katika magunia na kushindilia ambapo kipimo hicho sio sahihi na hakilengi kumwinua mkulima hivyo basi mradi wa Faida Mali unapowasaidia kutafuta masoko uangalie na vipimo vinavyotumika katika kununua zao hilo.

Kwa upande wake Meneja wa Mradi wa Faida Mali Mkoa wa Singida Christopher Mkondya amesema ili wakulima wazalishe kibiashara watawasaidia kupata mbegu bora na ya kisasa, kupata huduma mbalimbali za ugani, masoko na kuwaunganisha wakulima hao na huduma za kifedha.

Mkondya amesema kwa kushirikia na Autainsurance watawasaidia wakulima kupata elimu ya faida za bima na hivyo watakata bima ya mazao yao ili wakipata majanga yoyote kama vile moto, mafuriko, au mbegu kutoota wataweza kufidiwa na kuepuka hasara.

Ameongeza kuwa kupitia watoa huduma wao ambao ni Ersoko wamejipanga kutoa elimu kwa wakulima hasa kwa kuwatumia ujumbe mfupi wa maneno ambapo mkulima atapata taariza zote za kilimo cha alizeti kulingana na eneo alipo kwa kumuelekeza mbinu za kulima kisasa, muda wa kupanda, aina ya mbolea na taarifa za masoko ya mazao yake.




 Mwenyekiti wa chama cha Wakulima wa Alizeti Mkoa wa Singida Athumani Sima akisisitiza jambo katika kikao cha wadau wa kilimo cha alizeti, kilichoandaliwa na Mradi wa Faida Mali.


 Meneja wa Mradi wa Faida Mali Mkoa wa Singida Christopher Mkondya akiandika maoni ya wakulima wa alizeti wakati wa majadiliano katika kikao cha wadau wa kilimo cha alizeti.



 Baadhi ya wakulima wa alizeti wakiandika baadhi ya maelekezo, mapendekezo na maoni yaliyotolewa katika kikao cha wadau wa kilimo cha alizeti, kilichoandaliwa na Mradi wa Faida Mali.



Mkulima wa alizeti Kutoka kata ya Kinampundu Wilaya ya Mkalama Samwel Laida akifafanua jambo katika kikao cha wadau wa kilimo cha alizeti, kilichoandaliwa na Mradi wa Faida Mali.



 Mkurugenzi wa Faida Mali Mkoa wa Singida Tom Silayo akiwaelezea wakulima wa alizeti mambo ambayo mradi huo utayatekeleza.



 Afisa Kilimo Sekretarieti ya Mkoa wa Singida Mashaka Mlangi na Afisa Maendeleo ya Jamii Patrick Kassango wakichukua maoni ya wakulima walioudhuria kikao cha wadau wa kilimo cha alizeti kwa ajili ya utekelezaji na ufuatiliaji.

Tuandikie Maoni Yako Hapa

Post a Comment

0 Comments