Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma Dkt.
Laurean Ndumbaro amewataka viongozi na watumishi wote nchini kuzingatia nidhamu
kama msingi wao wa utendaji kazi pamoja na kanuni na maadili ya utumishi wa
umma ili utumishi wao uweze kuwa mzuri.
Dkt. Ndumbaro ameyasema hayo alipokutana na watumishi Mkoani
Singida na kusikiliza matatizo, kero, changamoto pamoja na kupata maoni ya
namna ya kuboresha utumishi wa umma kama sehemu ya maadhimisho ya wiki ya
utumishi wa umma nchini.
Amesema kila mtumishi anapaswa kufanya kazi kwa bidii na kwa
nidhamu ya hali huku akiwasisitiza viongozi hasa wa watumishi wa umma
kuwasikiliza watumishi wao pale wanapotoa maoni yao bila kuyapuuzia au
kuwakatisha tamaa kwa vitisho.
“Ukiwa kiongozi unapaswa uweze kuishi na kila aina ya mtu, kuna
watumishi wengine hawawezi kufichaficha mambo ukikosea wanakusema bila kupepesa
maneno, wengine ni waoga hawawezi kukueleza wazi ila wanatumia mbinu mbali
mbali, ukiwa kama kiongozi uwe tayari kupokea ushauri ili uweze kuboresha utendaji
wako”, amesisitiza Dkt Ndumbaro.
Dkt Ndumbaro amewaasa viongozi hao kuwapongeza watumishi
wanaofanya kazi kwa bidii na wenye nidhamu ili iwe motisha kwa wale wavivu huku
akiwataka kuwachukulia hatua wale wazembe na ambao hawataki kufuata kanuni na maadili
ya utumishi wa umma.
“Unakuta mtumishi anajituma anafanya kazi kwa bidii, ana nidhamu
na ni mbunifu lakini wewe kiongozi wake unamuangalia tu bila hata ya
kumpongeza, hiyo inakatisha tamaa, inatakiwa umpongeze sio lazima umpe fedha
hata barua tu ya kutambua utendaji wake itampa hamasa yeye na wenzake. Lakini
pia kuna mwingine anakuwa hatekelezi wajibu wake unamtazama tu, hapo
utawakatisha tamaa hata wale wachapakazi, amesema.
Aidha amewapongeza watumishi wenye vyeti halali huku akieleza
kuwa zoezi la uhakiki wa watumishi bado ni endelevu ili kuhakikisha watumishi
wanaobaki serikalini ni wale wanaostahili tu huku akiwashauri watumishi
kuhakikisha wanasafisha taarifa zao muhimu ziwe halali na sahihi.
Naye Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Angelina Mageni Lutambi
amemshukuru Katibu Mkuu Utumishi kwa kuwatembelea watumishi wa Mkoa wa Singida
na kusikiliza changamoto pamoja na maoni yao huku akiahidi kwa niaba ya
watumishi kuwa wataendelea kuchapa kazi kwa bidi na nidhamu.
Dkt Lutambi amesema watumishi Mkoani Singida wanaadhimisha wiki
ya Utumishi wa Umma kwa kufanya kazi kwa bidi pamoja na kuongeza muda wa
kufanya kazi kutoka saa tisa na nusu mchana mpaka saa kumi na nusu jioni ili
kutoa muda zaidi wa kuwahudumia wananchi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba
Linno Mwageni amemshukuru Katibu Mkuu Utumishi kuutembelea Mkoa wa Singida na
kutoa maoni yake kuwa ili kuboresha utendaji hasa wa serikali za Mitaa inabidi
serikali iwaajiri watendaji wa vijiji na kata wa kutosha.
Mwageni amesema watekelezaji wa shughuli na miradi ya serikali
kwa ngazi ya mwananchi hasa ni watendaji wa vijiji na kata ambao kwa sasa ni
wachache hivyo serikali iwaajiri wa kutosha ili waweze kufuatili kwa ukaribu
miradi hiyo.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma Dkt.
Laurean Ndumbaro akizungumza na watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida
(hawapo pichani) kama sehemu ya maadhimisho ya wiki ya utumishi wa Umma.
Watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida wakimsikiliza
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma Dkt. Laurean Ndumbaro
alipowatembelea katika kuadhimisha wiki ya utumishi umma.
Afisa Elimu Taaluma Mkoa wa Singida Mwalimu Eva Mosha akitoa
maoni yake kwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma Dkt.
Laurean Ndumbaro aliwapotembelea watumishi wa Mkoa wa Singida katika
kuadhimisha wiki ya Utumshi wa Umma.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma Dkt.
Laurean Ndumbaro (katikati) akizungumza na watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
wa Singida (hawapo pichani) kama sehemu ya maadhimisho ya wiki ya utumishi wa
Umma kulia kwake ni Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Angelina Mageni Lutambi
na Kushoto kwake ni Afisa Utumishi kutoka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi
wa Umma Bw. Nsajigwa.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba Linno Mwageni
akimshukuru Katibu Mkuu Utumishi kuutembelea Mkoa wa Singida pamoja na kutoa
maoni yake ya kuboresha utumishi wa Umma.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma Dkt.
Laurean Ndumbaro akiandika maoni na changamoto za watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa
Mkoa wa Singida (hawapo pichani) kama sehemu ya maadhimisho ya wiki ya utumishi
wa Umma kulia kwake ni Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Angelina Mageni
Lutambi.
0 Comments