Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida limemfikisha mahakamani kijana mmoja, Sendama Mabula Singu mwenye umri wa miaka 24, anayejishughulisha na uchimbaji mdogo wa dhahabu katika eneo la Makarunda, Kijiji cha Sambaru, Kata ya Mang’onyi wilayani Ikungi.
Mtuhumiwa huyo anadaiwa kusambaza taarifa zisizo za kweli akidai kuwa alihifadhiwa na mtu mmoja aitwaye Richard Michael Isango, mkazi wa Maili Sita Manispaa ya Singida, ambaye pia ni Mkurugenzi wa kampuni binafsi ya ulinzi ya GSY Service and Security Company, na kwamba alifanyiwa tukio la kuondolewa sehemu zake za siri—madai yaliyosababisha taharuki kubwa kwa wananchi.
Kwa mujibu wa Polisi, tukio hilo liliripotiwa Aprili 9, 2026 majira ya saa 12 jioni, ambapo uchunguzi ulianzishwa mara moja na kumpelekea kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo na kuhojiwa katika Kituo cha Polisi Ikungi.
Baada ya uchunguzi wa kina uliofanywa kwa ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na madaktari wa Hospitali ya Wilaya ya Ikungi, ilibainika kuwa mtuhumiwa huyo hakuwa na madhara yoyote na alikuwa na afya njema, jambo lililothibitisha kuwa taarifa alizotoa zilikuwa za uzushi.
Jeshi la Polisi lilikamilisha uchunguzi na kumfikisha mahakamani Aprili 10, 2026 kwa hatua zaidi za kisheria.
Katika hatua nyingine, Polisi Mkoa wa Singida limewataka wananchi kuacha kuamini na kusambaza taarifa zisizo na ukweli pamoja na imani za kishirikina, na badala yake kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola ili kudhibiti vitendo vya upotoshaji vinavyoweza kuleta taharuki katika jamii.




0 Comments