
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema
Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu
Hassan imeendelea kuthamini na kutambua mchango wa sekta binafsi katika
kuimarisha ustawi wa jamii ya Watanzania.
Ameyasema hayo alipomuwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kufungua
hospitali ya Saifee Tanzania jijini Dar es Salaam. Amesema sekta binafsi
zimekuwa zikiunga mkono jitihada za Serikali katika kutoa huduma mbalimbali kwa
wananchi.
Waziri Mkuu amesema mchango wa sekta
binafsi katika eneo la kutoa huduma kwa wananchi ni mkubwa na unadhihirika
kupitia huduma mbalimbali wanazozitoa ambazo ni pamoja na huduma za afya, elimu, mawasiliano na maji.
Amesema kwa upande wa sekta ya Afya, Serikali
inatekeleza kwa vitendo Sera ya Ubia kwa kufanya kazi pamoja na baadhi ya vituo
vya kutolea huduma ya afya vinavyomilikiwa na sekta binafsi.
Pia, Waziri Mkuu amesema amefarijika na huduma
zinazotolewa na hospitali hiyo zikiwemo za upasuaji wa moyo, mgongo, ubongo kwa
kutumia teknolojia za kisasa za kitabibu na pia kuweka vipandikizi (implants)
kwenye matibabu ya mifupa.
“Ni matumaini yangu kuwa Taasisi ya
Saifee itasaidia kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda nje ya nchi na kupunguza
gharama kwa wananchi na Serikali kwa ujumla, hivyo uwekezaji huu una manufaa makubwa sana kwa
Taifa.”
Amesema Hospitali ya Saifee na
nyingine kama hizo nchini, ni nyenzo muhimu katika kuiharakisha Tanzania
kuelekea kuwa kitovu cha utalii Tiba katika Ukanda wa Afrika Mashariki, Kati na
Kusini pamoja na Visiwa vya Bahari ya Hindi.
Kwa upande wake, Waziri wa Afya, Ummy
Mwalimu amesema wataendelea kuwa wabunifu na kushirikiana na sekta binafsi
katika kuboresha huduma za afya kwa Watanzania. Tanzania kuna vituo zaidi ya
12,000 vya kutolea huduma za afya kati yake asilimia 60 ni vya Serikali na
asilimia 40 vinamilikiwa na sekta binafsi.
Pia, Waziri Ummy ametumia fursa hiyo
kutoa wito kwa Watanzania wazingatie ulaji unaofaa pamoja na kufanya mazoezi
ili kuepukana na magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo ya moyo na kisukari.
0 Comments