Uchunguzi dhidi ya waamuzi Martin Saanya,
Samuel Mpenzu (mechi ya Yanga Vs Simba), Thomas Mkombozi (mechi ya Coastal
Union Vs KMC) na Rajab Mrope (mechi ya Mbeya City na Yanga) umekaribia
kukamilika.
Hatua ya mwisho ya uchunguzi huo ni wao kufika
mbele ya Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi (Kamati ya Saa 72) ambapo
watahojiwa ili kutoa ufafanuzi katika masuala mbalimbali yaliyojitokeza katika
taarifa zao.
MATUKIO
YA LIGI KUU
Mchezo namba 90 (Simba Vs Toto Africans).
Klabu ya Toto Africans imepewa onyo kali kutokana na timu yake kuchelewa kufika
uwanja kwa dakika saba. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(48) ya Ligi
Kuu.
Mechi namba 99 (Mwadui Vs Simba). Klabu zote mbili
zimepigwa faini ya sh. 500,000 kila moja kwa timu zao kuingia uwanjani kwa
kutumia mlango wa washabiki, kitendo ambacho ni kinyume na Kanuni ya 14(14) ya
Ligi Kuu. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 14(48).
Mechi namba 101 (Ruvu Shooting Vs Stand Utd).
Ndanda FC imepigwa faini ya sh. 500,000 kwa kosa la timu yake kuingia uwanjani
kwa kutumia mlango usio rasmi, kitendo ambacho ni kinyume na Kanuni ya
14(14) ya Ligi Kuu. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 14(48).
Nayo Ruvu Shooting ambayo ilikuwa uwanja wa
nyumbani, imepigwa faini ya sh. 500,000 kwa kuchelewa kuingia uwanjani kwa
dakika 15. Kitendo hicho ni ukiukwaji wa Kanuni ya 14(9) ya Ligi Kuu, na adhabu
ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(48).
Mechi namba 104 (JKT Ruvu Vs Ndanda). Klabu ya
Stand United imepewa onyo kali baada ya wachezaji wake kufanya vurugu wakitaka
kuingia uwanjani bila ya kuwa na uthibitisho kuwa wao ni wachezaji wa timu hiyo
wakati wa mechi kati ya JKT Ruvu na Ndanda iliyofanyika Uwanja wa Mabatini
mkoani Pwani. Kitendo hicho ni kinyume na Kanuni ya 42(1).
Mechi namba 112 (Majimaji Vs JKT Ruvu).
Daktari wa JKT Ruvu, Abdullah Yusuf amefungiwa miezi mitatu, na kupigwa faini
ya sh.
300,000 baada ya kutolewa kwenye benchi la
ufundi kwa kusababisha usumbufu kwa Mwamuzi Msaidizi Namba Moja, na kuwatolea
maneno machafu Mwamuzi na Mwamuzi wa Akiba. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya
41(2).
Mtaalamu wa viungo wa JKT Ruvu, George Minja
amefungiwa miezi mitano na kupigwa faini ya sh. 300,000 kwa kumvamia Mwamuzi
akitaka kumpiga, na pia kutoa lugha ya matusi kwa waamuzi baada ya mechi hiyo.
Adhabu ni kwa mujibu wa Kanuni ya 41(2).
Nao wachezaji wa JKT Ruvu, Said Kipao jezi
namba moja, Samwel Kamuntu (22), Pela Mavuo (16) na paul Mhidzhe (23)
wamefungiwa mechi tatu na faini ya sh. 500,000 kila mmoja kwa kuwatukana
waamuzi baada ya mchezo kumalizika. Adhabu imezingatia Kanuni ya 37(7).
Mechi namba 116 (Mbao FC Vs Azam FC). Kocha wa
Azam FC, Zeben Hernandez amefungiwa mechi tatu na faini ya sh. 500,000 baada ya
kuondolewa kwenye benchi la ufundi (ordered off) kwa kukataa kuheshimu mipaka
ya eneo la ufundi (technical area) katika mechi hiyo. Adhabu imezingatia Kanuni
ya 40(11).
Mechi namba 117 (Ndanda Vs Stand Utd). Katika
mechi hiyo kadri muda ulivyokuwa ukienda ball boyz walichelewesha kurudisha mipira
uwanjani, na mbaya zaidi mipira ilikuwa ikifichwa kiasi cha kubaki miwili kati
ya sita iliyokuwepo. Msimamizi wa Kituo ameandikiwa barua ili ahakikishe suala
hilo halijitokezi tena.
Mechi namba 59 (Yanga Vs Ruvu Shooting). Timu
ya Ruvu Shooting imepewa onyo kali kwa kuchelewa kuingia uwanjani kwa dakika
12, jambo ambalo ni kinyume cha Kanuni ya 14(14) ya Ligi Kuu.
Kocha wa Yanga, Hans van Pluijm amepigwa faini
ya sh. 500,000 na kufungiwa mechi tatu baada ya wakati wa mapumziko kuwazonga
waamuzi na kuwatolea maneno ya kashfa. Pia baada ya mechi kumalizika alikwenda
kwenye chumba cha waamuzi na kuwatolea maneno ya kashfa. Adhabu hiyo ni kwa
uzingativu wa Kanuni ya 40(1).
Klabu ya Yanga imepigwa faini ya sh. 500,000
baada ya washabiki wake kuwazonga waamuzi na kuwatolea maneno ya kashfa
walipokuwa wakiingia vyumbani wakati wa mapumziko. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa
Kanuni ya 42(1).
Mechi namba 60 (Tanzania Prisons Vs Simba).
Klabu ya Simba imepigwa faini ya sh. 500,000 kutokana na timu yake kuchelewa kwenye
kikao cha maandalizi ya mechi (pre match meeting) na kufika wakati taratibu
zote za msingi zikiwa zimemalizika. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya
14(3) ya Ligi Kuu.
Klabu zote (Tanzania Prisons na Simba)
zimepigwa faini ya sh. 500,000 kila moja kwa timu zao kuingia uwanjani kwa
milango isiyo rasmi. Kitendo hicho ni kinyume cha Kanuni ya 14(14), na adhabu
imezingatia Kanuni ya 14(48).
Pia Tanzania Prisons imepigwa faini ya sh.
500,000 baada ya gari la Jeshi la Magereza namba MT 0084 aina ya Toyota Land
Cruiser Pick Up likiwa na watu 15 kuingia uwanjani kwa nguvu, na kusababisha
kupigwa na kuumizwa kwa mlinzi wa getini. Adhabu ni kwa mujibu wa Kanuni ya
42(1).
Kamishna wa mechi hiyo Jimmy Lengwe kutoka
Morogoro amepewa onyo kali kwa kutoripoti baadhi ya matukio ya wazi yaliyotokea
kabla ya mechi hiyo kuanza.
MATUKIO
YA LIGI DARAJA LA KWANZA
GROUP
A
Mechi namba 17 (Polisi Dar Vs Ashanti
Utd). Kiongozi wa Polisi Dar, Ulimwengu Hamimu amefungiwa miezi sita na kupigwa
faini ya sh.
200,000 kwa mujibu wa Kanuni ya 41(2).
Kiongozi huyo alichukua mpira na kuupiga kwenye jukwaa la timu ya Ashanti Utd
na kutaka kumpiga Mwamuzi akiwa na mchezaji wake Pascal Theodory mwenye jezi
namba 15. Mchezaji huyo amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 100,000.
Mechi namba 19 (Pamba Vs African Sports).
Klabu ya African Sports imepewa onyo kali kwa kuchelewa kwenye kikao cha
maandalizi ya mechi (pre match meeting) kwa dakika nne, na kufika na viongozi
watatu badala ya wanne.
Mchezaji Shaban Kimaro amefungiwa mechi sita
na kupigwa faini ya sh. 300,000 baada ya kumpiga kichwa Mwamuzi Msaidizi Namba
Mbili. Mwamuzi alimtoa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa hilo alilolifanya dakika
83. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 24(6) ya Ligi daraja la Kwanza.
Naye Salum Omari pia wa African Sports
amefungiwa mechi tatu na faini sh. 300,000. Akiwa mchezaji wa akiba aliingia
uwanjani kwa nia ya kutaka kumshambulia Mwamuzi, lakini Polisi walimuwahi na
kumtoa.
Mechi namba 20 (Kiluvya Utd Vs Mshikamano).
Mchezaji Ayoub Upatu wa Mshikamano amesimamishwa na suala lake limepelekwa
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF kwa hatua zaidi baada ya Kiluvya
Utd kuwasilisha pingamizi dhidi yake kuwa ni mchezaji wao, kwani wana leseni
yake. Katika leseni ya Kiluvya Utd ametumia jina la Ayoub Kassim Lipati.
Mechi namba 25 (Ashanti Utd Vs Lipuli). Kamati
imetupa malalamiko ya timu ya Lipuli dhidi ya Ashanti Utd kuwa katika mechi yao
ilimchezesha mchezaji Patrick James mwenye jezi namba 15 wakati akiwa na kadi
tatu za njano. Kamati imebaini wakati James akicheza mechi hiyo alikuwa na kadi
mbili za njano, na si tatu.
Mechi namba 27 (Kiluvya Utd Vs Friends
Rangers). Kocha Msaidizi wa Friends Rangers, Fadhili Ndumba amefungiwa mechi
mbili na faini ya sh. 300,000 baada ya kutolewa kwenye benchi na Mwamuzi kwa
kutoa lugha ya matusi kwa Mwamuzi Msaidizi Namba Moja. Adhabu hiyo ni kwa
mujibu wa Kanuni ya 40(11) ya Ligi Daraja la Kwanza.
GROUP
B
Mechi namba 23 (Kurugenzi Vs Kimondo).
Viongozi wa Kimondo, Eric Ambakisye, Selestine Mashenzi, na Mussa Minga
wamefungiwa miezi sita, na kupigwa faini ya sh. 500,000 kila mmoja kwa
kuwafuata waamuzi hotelini baada ya mechi ambapo walimpiga Mwamuzi Mussa
Gabriel na kumjeruhi wakishirikiana na baadhi ya wachezaji wao.
Wachezaji waliohusika katika tukio hilo ambapo
wamefungiwa mechi sita na faini ya sh. 500,000 kila mmoja ni; January Daraja
Mwamlima, Daniel Douglas Silvalwe, Abiud Kizengo na Monte Stefano Mwanamtwa.
Adhabu zote ni kwa mujibu wa Kanuni ya 24(6) ya Ligi Daraja la Kwanza.
GROUP
C
Mechi namba 23 (Alliance Vs Mvuvumwa).
Kocha Msaidizi wa Mvuvumwa, Ezekiel Chobanga amefungiwa mechi mbili na kupigwa
faini ya sh. 300,000 baada ya kutolewa kwenye benchi la ufundi dakika ya 59 kwa
kumtolea lugha chafu Mwamuzi. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 40(11) ya Ligi
Daraja la Kwanza.
Mechi namba 24 (Polisi Dodoma Vs Rhino
Rangers). Mchezaji Sameer Mwishehe wa Rhino Rangers amefungiwa mechi tatu na
kupigwa faini ya sh. 500,000 kwa kumrushia Mwamuzi chupa ya maji baada ya
mchezo kumalizika. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 37(7) ya Ligi Daraja
la Kwanza.
Mechi namba 25 (Polisi Dodoma Vs Mgambo
Shooting). Kocha wa Mgambo, Athuman Kairo amefungiwa mechi mbili na kupigwa
faini ya sh. 300,000 baada ya kutolewa kwenye benchi la ufundi kwa kosa la
kumshambulia kwa maneno Mwamuzi wa Akiba. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya
40(11).
Mechi namba 28 (Alliance Vs Singida Utd).
Baada ya Alliance kupata bao, watu wa huduma ya kwanza walipokuwa wakiitwa
kuingia uwanjani, walikuwa wanakwenda kwa kupoteza muda. Msimamizi wa Kituo
ameandikiwa barua ya kuwakumbusha watu wa huduma ya kwanza kutekeleza majukumu
yao wawapo uwanjani, na kuhakikisha kuwa tukio la aina hiyo halitokei tena.
LIGI
DARAJA LA PILI
GROUP
A
Mechi namba 4 (Bulyanhulu Vs Green Warriors).
Mechi hiyo haikuchezwa kutokana na wachezaji wa Bulyanhulu kutokuwa na leseni,
na vilevile kutokuwepo mawasiliano kati ya Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) na Kamishna wa mechi hiyo juu ya tatizo hilo. Hivyo, mechi hiyo
itapangiwa tarehe nyingine na kuchezwa katika uwanja huru (neutral ground).
Mechi namba 7 (Mji Mkuu Vs Bulyanhulu). Mechi
hiyo haikuchezwa baada ya wachezaji wa Bulyanhulu wakiongozwa na Katibu Mkuu
wao Alphonce Innocent kugomea wakitaka wachezaji watano wa Mji Mkuu ambao
hawakuwa na leseni, lakini walikuwa na utambulisho maalum kutoka TFF wasicheze.
Licha ya Kamishna kuwataka wacheze na baadaye
wawasilishe malalamiko yao kwake, walikataa huku Katibu wao Innocent akimzonga
Kamishna na kumtukana. Bulyanhulu imepoteza mechi hiyo kwa kusababisha
ivurugike kwa kuzingatia Kanuni ya 29(4) ambapo pia imepigwa faini ya sh.
1,000,000. Mji Mkuu imepewa ushindi wa pointi tatu na mabao matatu.
Pia Katibu Mkuu wa Bulyanhulu, Aplhonce
Innocent amefungiwa miezi sita kutojihusisha na shughuli yoyote inayohusu mpira
wa miguu. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 29(6) ya Ligi Daraja la
Kwanza.
GROUP
B
Mechi namba 1 (African Wanderers Vs AFC).
Klabu ya African Wanderers imepigwa faini ya sh. 200,000 kwa kutohudhuria kikao
cha maandalizi ya mechi licha ya kuwa ni wenyeji. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa
Kanuni ya 14(3) ya Ligi Daraja la Pili.
Mechi namba 5 (African Wanderers Vs
Kitayosce). Wachezaji Ally Rashid na Israel Said wa African Wanderers
wamefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 300,000 kila mmoja kwa Mwamuzi
kuwatoa kwa kadi nyekundu baada ya kwenda nje ya uwanja na kupigana na
washabiki. Adhabu imezingatia Kanuni ya 37(3) ya Ligi Daraja la Pili.
Mechi namba 12 (JKT Oljoro Vs African
Wanderers). Mechi hiyo haikuchezwa baada ya kutokea mkanganyiko wa mawasiliano
kati ya African Wanderers na ofisi ya Bodi ya Ligi, hivyo itapangiwa tarehe
nyingine.
GROUP
D
Mechi namba 2 (Namungo Vs Sabasaba). Baada ya
Namungo kufunga bao, washabiki wa timu hiyo waliingia uwanjani kushangilia.
Klabu hiyo pamoja na Msimamizi wa Kituo wamepewa onyo kali kuhakikisha tukio
hilo halitokei tena. Pia sehemu kubwa ya uwanja huo hauna nyasi, hivyo klabu
husika imetakiwa kuhakikisha nyasi zinapandwa kabla ya kuanza mzunguko wa pili.
Mechi namba 9 (Mbarali United Vs Mkamba Rangers).
Kamati imefuta kadi nyekundu aliyoonyeshwa mchezaji David Francis mwenye jezi
namba 5 wa Mkamba Rangers baada ya kubaini kuwa ilitolewa kimakosa.
MIN
34/MSC/2016 - MAOMBI YA MVUVUMWA KUCHEZA SHINYANGA
Kamati imeridhia maombi ya timu ya Mvuvumwa kuhamishia
mechi zake za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kwenye Uwanja wa Kambarage mjini
Shinyanga kutoka Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma. Hivyo, kuanzia
Mzunguko wa Pili wa SDL, mechi za Mvuvumwa zitachezwa mjini Shinyanga.
0 Comments