Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa amewataka wakuu
wa mikoa na wakuu wa wilaya nchini kufanya mapitio ya vikundi vyote vya Jogging
katika halmashauri zao na waviweka kwenye mipango ya maendeleo.
“Nendeni mkawasikilize ili muwatambue, muwashike
mkono na muwaongoze kushiriki katika kukuza uchumi wao binafsi kupitia miradi
mbalimbali kwenye halmashauri”
Amesema hayo leo (Jumapili, Juni 16, 2024) wakati
alipoongoza tamasha kubwa la jogging lililoandaliwa na kituo cha Televisheni na
Radio cha EFM. Jogging hiyo la Kilomita tano ilianzia katika viwanja vya
Tanganyika Packers, Kawe hadi Tangi Bovu mbezi na kurejea viwanja vya
Tanganyika Packers jijini Dar es Salaam.
Aidha, Waziri Mkuu ametoa wito kwa viongozi wa
vikundi vya jogging kote nchini kuendeleza vikundi hivyo na kwenda kuvisajili
kwenye halmashauri zao ili waweze kutengeneza mazingira ya kushiriki kwenye
fursa nyingine za kiuchumi
“Mnaweza kutumia jogging yenu ambayo mmeisajili,
kuwa kikundi cha ushirika, kikundi cha uwekezaji, kikundi cha biashara ikiwa mmejisajili
kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii na Idara ya Utamaduni na Michezo ya kila
halmashauri”
Katika Hatua nyingine Mheshimiwa Majaliwa amesema
kuwa moja ya mikakati ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.
Samia Suluhu Hassan ni kuhamasisha watanzania kushiriki katika mazoezi ili
kukabiliana na magonjwa yasiyoambukizwa.
“Tuendelea kumuunga mkono Rais Dkt. Samia kwa
kuunda vikundi mbalimbali vya michezo”
Kwa upande wake, Waziri wa Afya Ummy Mwalimu
amesema kuwa madhara ya kutofanya mazoezi ni makubwa na takwimu za wizara hiyo
hazioneshi mwenendo mzuri katika magonjwa ya moyo na kisukari
“Hata kama una kisukari au shinikizo na juu la damu, ukifanya
mazoezi unazuia usiende katika hatari kubwa ikiwemo ya kukatwa viungo, kinga ni
bora kuliko tiba”.
0 Comments