Na Mwandishi wetu
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameagiza
taarifa maalum ya udhibiti wa vitendo vya uvuvi haramu iwasilishwe kabla ya
Wizara ya Mifugo na Uvuvi haijawasilisha hotuba ya bajeti ya mwaka 2024/2025.
Ametoa agizo hilo leo (Jumapili,
Aprili 21, 2024) katika hafla ya uzinduzi wa boti maalum kwa ajili ya
kukabiliana na vitendo vya kihalifu katika bahari hapa nchini iliyofanyika
bandarini jijini Dar es Salaam.
“Taarifa kuhusiana na shughuli maalum
ya udhibiti wa vitendo vya uvuvi haramu katika ukanda wa Bahari kuu iwasilishwe
kabla ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi haijawasilisha hotuba ya bajeti ya mwaka
2024/2025,” amesema.
Ameishukuru Serikali ya Japan kwa
kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kufanikisha mipango ya
maendeleo ambayo imechangia dola za Marekani 500,000 kwenye ununuzi wa boti
hiyo. “Ninaiomba Serikali ya Japan isichoke kutusaidia ili tuweze kukamilisha
utekelezaji wa mikakati iliyopo katika eneo hili la kukabiliana na uhalifu
nchini,” amesema.
Vilevile, amelishukuru Shirika la Maendeleo
la Umoja wa Mataifa (UNDP) kwa kuchangia dola za Marekani 400,000 kwenye mradi
huo. “Mchango wenu tunauthamini sana, wakati wote mmekuwa mkishirikiana nasi
katika maeneo mengi, kwa niaba ya wananchi na Serikali ya Tanzania
ninawashukuru sana,” amesema.
Mapema, akitoa taarifa ya mradi huo mbele ya Waziri
Mkuu, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Ummy
Nderiananga alieleza kuwa ununuzi wa boti hiyo ni sehemu ya mafanikio ya
utekelezaji wa Mradi wa Kukabiliana na Vitendo vya Kihalifu katika Bahari na
Maziwa Makuu unaotekelezwa na Serikali.
Alisema mapambano hayo yatahusisha
kuimarisha juhudi za kukabiliana na vitendo vya kihalifu kama vile uvuvi
haramu, uhamiaji haramu, uharamia, usafirishaji wa dawa za kulevya na
utoroshwaji wa nyara za Serikali.
Akieleza sifa za boti hiyo alisema:
“Ni boti ni mpya, ya kisasa yenye uwezo mkubwa wa kuhimili utekelezaji wa
majukumu ya doria. Boti hii ya doria imepewa jina la Patrol Boat Sailfish (PB
Sailfish).”
Amesema uwepo wa boti hiyo utaleta
mageuzi makubwa kwenye ulinzi na usalama wa baharini kwani itawezesha kufanya
doria na kaguzi kwenye maji ya Tanzania. “Itafanya utafutaji na uokozi pindi
zikitokea ajali baharini na kuimarisha ulinzi kwenye pwani yetu kwa kuwa
imewekewa mitambo maalum ya silaha pamoja na mtambo maalum wa kuzima moto… boti
hii ni mwarobaini wa kuhakikisha pwani ya Tanzania iko salama.”
Kwa upande wake, Balozi wa Japan
nchini, Yasushi Misawa amesema nchi yake itaendelea kushirikiana na Serikali ya
Tanzania katika mapambano hayo na kueleza umuhimu wa mradi kuwa utaimarisha uwezo
wa Tanzania wa kuzuia shughuli haramu ndani ya bahari ya Tanzania.
Alitumia fursa hiyo kueleza kuwa nchi
yake itaendelea kuimarisha mahusiano wa kirafiki uliopo baina ya nchi hizo
mbili kwa zaidi ya miaka 60 tangu uhuru wa Tanzania. “Kwa mtazamo wa usafiri wa
majini, JICA imeamua kutoa fedha zaidi kwa ajili ya mradi wa ukaratbati wa
bandari ya Kigoma. Japan pia kwa muda mrefu imekuwa ikiisaidia Tanzania katika
kukuza sekta ya uvuvi,” alisema Balozi Misawa.
Naye, Waziri wa Mifugo na Uvuvi,
Abdallah Ulega ameishukuru Serikali kwa kupatikana kwa boti ya doria kwenye
bahari na maziwa makuu kwa sababu itatatua changamoto ya uhalifu.
Ameishukuru Serikali kwa kupambana na
milipuko baharini pamoja na kuwakabili wahusika wa vilipuzi ambapo hadi sasa watuhumiwa
wapatao 24 wamekwishakamatwa. “Kati ya hao, 13 ni wasambazaji wa vilipuzi, 10
ni wavuvi na mmoja ni mfadhili wao,” alisema.
Amesema jitihada zinazafanyika
kudhibiti vitendo hivyo katika maeneo yote ya ukanda wa bahari ya Hindi na
baadaye nguvu zitaelekezwa kwenye maziwa makuu.
Akitoa taarifa kuhusu ufanisi boti
hiyo, Mkurugenzi wa Idara ya Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Brigedia Jenerali
Hosea Ndagala alisema boti hiyo ina uwezo kukimbia kwa kasi ya km. 47 kwa saa
(nautical miles 25), inaweza kubeba wahalifu 20 kwa pamoja, inaweza kutumika
kubebea wagonjwa (ambulance), kuzima moto na kwenye shughuli za uokoaji.









0 Comments